Iran yasisitiza udharura wa kuwa na uhusiano mwema na nchi zote duniani
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kislamu ya Iran imetoa taarifa kwa mnasaba wa maadhimisho ya mwaka wa 40 wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na kusisitiza kuwa: Kuwa na uhusiano wa heshima, wa amani na wa pande kadhaa na nchi za dunia ni miongoni mwa stratijia za Iran.
Taarifa iliyotolewa leo na wizara hiyo imesema kuwa, kushirikiana na kuwa na uhusiano wa heshima, wa amani, wa pande kadhaa na nchi mbalimbali duniani bila ya kufanya ubeberu wala kukubali ubeberu ni miongoni mwa stratijia za Iran zinazopewa kipaumbele katika siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tangu siku za mwanzoni mwa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeongeza kuwa, kipindi cha Alfajiri Kumi cha maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini ni kielelezo cha kusimama kidete na azma ya taifa kubwa na lenye historia na utamaduni wa miaka mingi.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran itaendelea kushikamana na misingi na thamani zilizokita mizizi za Mapinduzi ya Kiislamu na daima itatetea na kulinda maslahi ya nchi, wananchi na utawala wa Kiislamu kwa kutumia nyenzo mbalimbali kulingana na mazingira na wakati.
Katika taarifa hiyo Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetangaza tena utiifu wake kwa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu na taifa kubwa la Iran na kuwataka wananchi kushiriki kwa wingi katika sherehe za tarehe 11 Februari za kuadhimisha kutimia miaka 40 ya Mapindunzi ya Kiislamu.
Jumatatu ya tarehe 11 Februari Wairani wataadhimisha miaka 40 tangu Mapinduzi ya Kiislamu yapate ushindi hapo mwaka 1979 baada ya kuung'oa madarakani utawala wa kifalme katika harakati iliyoongozwa na hayati Imam Ruhullah Khomeini.