Kongamano la Warsaw halitaweza kupunguza nguvu za Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i51505-kongamano_la_warsaw_halitaweza_kupunguza_nguvu_za_iran
Kamanda Mkuu wa Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kongamano dhidi ya Iran ambalo linaandaliwa kwa pamoja na Marekani pamoja na Poland mjini Warsaw halitaweza kupunguza nguvu za Jamhuri ya Kiislamu au kubadilisha sera zake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 12, 2019 10:13 UTC
  • Kongamano la Warsaw halitaweza kupunguza nguvu za Iran

Kamanda Mkuu wa Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kongamano dhidi ya Iran ambalo linaandaliwa kwa pamoja na Marekani pamoja na Poland mjini Warsaw halitaweza kupunguza nguvu za Jamhuri ya Kiislamu au kubadilisha sera zake.

Meja Jenerali Mohammad Baqeri Mwenyekiti wa Baraza la Wakuu wa Majeshi ya Iran amepuuzilia mbali kongamano hilo ambalo linaanza Jumatano katika mji mkuu wa Poland, Warsaw na kusema halina maana. Baqeri amesema kuwa Poland imeahidi kuwa kongamano hilo ambalo linadaiwa kuwa ni la usalama Mashariki ya Kati halitakuwa na ajenda iliyo dhidi ya Iran. Pamoja na hayo, Meja Jenerali Baqeri amesema, pasina kujali iwapo mkutano wa Warsaw utakuwa na ajenda dhidi ya Iran au la, hakuna shaka kuwa utafeli katika kuathiri sera na nguvu za Jamhuri ya Kiislamu. Amesema Iran inasubiri kuona iwapo wakuu wa Poland watatekeleza ahadi zao au la.

Mkutano huo wa kimataifa unapangwa kufanyika Februari 13 na 14 ikiwa ni sehemu ya njama za Marekani za kuishinikiza Iran kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo amesema mkutano huo utalenga kujadili kile alichosema ni "uthabiti, amani, uhuru na usalama Mashariki ya Kati na hilo linajumlisha kuhakikisha kuwa Iran haiwi na nafasi haribifu."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo

Baada ya kukosolewa kutokana na kauli hiyo dhidi ya Iran, Naibu Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa mkutano huo hautakuwa jukwaa la kuihujumu au kuiharibia jina Iran.  Tayari mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema hatahudhuria mkutano huo wa Warsaw kama ambavyo mawaziri wengi wa Umoja wa Ulaya pia wataususia. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema mkutano huo wa Warsaw umefeli hata kabla ya kuanza.