Iran yakosoa undumakuwili wa nchi za Magharibi kuhusu haki za binadamu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekosoa sera za nchi za Magharibi za uuzaji silaha na vigezo vya haki za binadamu vilivyojaa undumakuwili.
Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameyasema hayo katika mkutano na waandishi habari pembizoni mwa Kongamano la Usalama la Munich nchini Ujerumani. Akijibu swali kuhusu tishio la Ufaransa la kuiwekea Iran vikwazo kutokana na mpango wake wa makombora ya kujihami, Zarif amesema: "Katika vita vya miaka minane vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran, utawala wa Iraq ulikuwa unatumia ndege za kivita za Ufaransa, silaha za kemikali za Ujerumani, vifaru vya Uingereza na ndege za kijasusi za Marekani za AWAC katika hali ambayo hakuna nchi yoyote iliyoipa Iran zana za kujihami."
Zarif aidha amezikosoa nchi za Magharibi kwa kuziuzia nchi za eneo idadi kubwa ya silaha na kusema: "Katika hali hii ambayo hakuna nchi yoyote inayoiuzia Iran hata ndege moja ya kivita, je, Jamhuri ya Kiislamu inapaswa kujihami kwa njia gani?"
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria azimio 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusema: "Hili azimio linahusu makombora ambayo yameundwa kwa ajili ya kubeba silaha za nyuklia na Jamhuri ya Kiislamu haina silaha yoyote ya nyuklia."
Zarif ameashiria pia madai ya baadhi ya nchi za Magharibi kuwa Iran inaunga mkono ugaidi na kusema: "Mwaka 1984, Marekani ilimuondoa Saddam, dikteta wa wakati huo wa Iraq, katika orodha ya ugaidi na ikaiingiza Iran katika orodha hiyo. Baada ya hapo Marekani ililiweka kundi la kigaidi la munafikina (MKO) katika orodha ya ugaidi na kisha ikaliondoa. Huu ni mchezo ambao unapapswa kusitishwa."
Kongamano la Usalama la Munich lilianza Ijumaa na kumalizika jana Jumapili ambapo limehutubiwa na viongozi wa ngazi za juu wakiwemo marais, mawaziri wa mambo ya nje na ulinzi na wakuu wa mashirika ya kimataifa katika mji wa Munich Ujerumani.