Afrika Kusini: Kujiondoa Marekani JCPOA hakuathiri uhusiano wetu na Iran
Balozi wa Afrika Kusini mjini Tehran amesema hatua ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA haitapunguza ushirikiano wa nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyuga za uchumi, biashara na utamaduni.
Vika Mazwi Khumalo ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Abbas Rezaei, Gavana Mkuu wa Isfahan, katikati mwa nchi na kuongeza kuwa, kuimarisha sekta ya utalii ni katika nyanja muhimu za kustawisha uchumi.
Huku akiashiria umuhimu wa kuanzisha safari ya moja kwa moja ya ndege kati ya Afrika Kusini na Iran, Balozi wa nchi hiyo ya Kiafrika mjini Tehran amebainisha kuwa, "Ingawaje kuna mipaka na changamoto katika kulifikia hilo, lakini nchi mbili hizi zinashirikiana kuondoa vizingiti hivyo."
Kwa upande wake, Abbas Rezaei, Gavana Mkuu wa Isfahan amesema nchi mbili hizi zina hamu na uwezo wa kubadilishana mawazo katika uga wa sayansi na teknolojia.
Afrika Kusini ni nchi ya pili kwa kuwa na uchumi mkubwa barani Afrika na imekuwa ikichukua hatua chanya za kuimarisha uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hasa baada ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
Akiwa mjini Pretoria mwezi Juni mwaka jana, Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema Afrika Kusini ni moja ya washirika wa karibu wa Tehran na kwamba serikali ya nchi hiyo daima imekuwa ikiunga mkono haki za wananchi wa Iran katika kadhia ya nyuklia kuanzia mwanzo wa mazungumzo hadi baada ya kufikiwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA.