Feb 22, 2019 12:23 UTC
  • Uwahabi; chanzo cha umwagikaji damu katika Ulimwengu wa Kiislamu

Meja Jenerali Qassim Suleimani, Kamanda MKuu wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran SEPAH, amesema kwamba magaidi wa kitakfiri wanaoungwa mkono na Saudi Arabia katika ardhi ya Pakistan wamekuwa tatizo kubwa la usalama kwa majirani wote wa nchi hiyo, zikiwemo India na Afghanistan na kwamba viongozi wa Pakistan wanapasa kulitambua vyema jambo hilo.

Akisisitiza Alkhamisi kuwa Uwahabi umesababisha mgawanyiko na umwagikaji damu mkubwa katika Ulimwengu wa Kiislamu, Qassim Suleimani amesema wazi kwamba serikali na watu wa Pakistan hawapaswi kutoa mwanya kwa fedha za Saudia kuwafikia kagaidi wa kitakfiri na kuifanya nchi hiyo kuhasimiana na uliwengu. Ukiwa unaungwa mkono na Marekani, utawala wa Saudi Arabia umekuwa na nafasi haribufu katika eneo zima la Mashariki ya Kati ambapo unafanya juhudi za kuwaunga mkono magaidi na kuvuruga usalama ndani ya mipaka ya Jamhuri ya  Kiislamu ya Iran. Kujiimarisha magaidi ambao wanaungwa mkono kifedha na Saudi Arabia katika maeneo ya mpaka wa Pakistan na Iran, kumewawezesha mara kadhaa kupenya na kutekeleza vitendo vya ugaidi katika ardhi ya Iran na hilo pia linatokana na kutokuwepo irada thabiti ya viongozi wa Pakistan kwa ajili ya kupambana na magaidi.

Meja Jenerali Qassim Suleimani

Jinai iliyotekelezwa na magaidi hao tarehe 13 mwezi huu wa Februari katika mkoa wa Sistan na Balochistan ambayo ilipelekea askari walinda-mpaka 27 wa Iran kuuawa shahidi inathibitisha wazi kujiimarisha kwa magaidi katika maeneo ya mpakani na kudhaminiwa kwao kifedha na Saudi Arabia ambayo huko nyuma imewahi kusema waziwazi kuwa itahamishia ghasia na machafuko ndani ya ardhi ya Iran. Gaidi aliyetekeleza mlipuko uliopelekea kuuawa askari hao alikuwa raia wa Pakistan jambo linalothibitisha wazi kutokuwepo irada ya kutosha kutoka kwa  viongozi wa Pakistan kwa ajili ya kupambana na ugaidi. Uwahabi una mizizi ya kina nchini Pakistan na madrasa za kidini ambazo zinaendeshwa kwa fedha za Saudia nchini humo zimebadilika kuwa vituo vya kuzalisha na kulea magaidi. Suala hilo liko wazi mbele ya walimwengu kadiri kwamba hivi karibuni Umoja wa Ulaya uliiweka Saudia katika orodha nyeusi ya nchi zinazofadhili ugaidi. Kuhusu hilo, Ro Khanna, mbunge katika Congress ya Marekani alisema wiki iliyopita kwamba watawala wa Saudia wanawapa magaidi wa al-Qaida nchini Yemen silaha za Marekani kwa ajili ya kuzitumia dhidi ya raia wa nchi hiyo masikini ya Kiarabu. Katika upande wa pili, Bahram Qassimi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa chanzo cha ugaidi ambao hii leo umeukumba ulimwengu na hasa eneo la Mashariki ya Kati, hakiko sehemu nyingine bali ni Saudia na fikra zake za kupindukia mipaka.

Mazishi ya wahanga wa ugaidi nchini Iran

Kutokana na kuenea kwa fikra hizo haribifu na zilizo dhidi ya mafundisho ya Uislamu katika madrasa za kidini zinazodhaminiwa kifedha na Saudia nchini Pakistan, nchi hiyo imebadilika na kuwa uwanja wa harakati za makundi ya kitakfiri. Kwa kuzingatia ukweli huo, viongozi wa Pakistan wanashauriwa wachukue hatua kali kidogo kwa ajili ya kuzuia magaidi hao hatari kupenya na kuingia katika ardhi ya Iran. Hatua ambazo hadi sasa zimechukuliwa na viongozi wa Islamabad kwa ajili ya kupambana na magaidi haziwaridhishi viongozi wa Iran na bila shaka kuimarishwa usalama katika mpaka wa pamoja wa nchi mbili kunahitajia juhudi zaidi kutoka serikali ya Pakistan, la sivyo, Iran imeazimia vilivyo kuchukua hatua za lazima kwa ajili ya kulinda usalama wa mipaka yake, kupambana na magaidi na kulipiza kisasi cha damu ya askari wake wa mpakani  waliouawa shahidi na magaidi huko Zahedan. Kama alivyosisitiza kamanda wa kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran italipiza kisasi kikali dhidi ya vibaraka wa kitakfiri ambao mikono yao imejaa damu ya vijana wa Iran. Iran ina nafasi muhimu katika kupambana na ugaidi unaodhaminiwa na  nchi za Magharibi na hasa Marekani na pia utawala wa Saudi Arabia. Mapambano halisi ya Iran dhidi ya makundi ya kigaidi yameonekana wazi katika nchi za Syria na Iraq ambapo yamepelekea kuporomoka kwa utawala wa magaidi wa Daesh katika nchi mbili hizo. Mapambano hayo ya Iran bila shaka ni onyo kali kwa waungaji mkono wa ugaidi ambao wanapasa kufahamu kwamba Iran haitambui mipaka yoyote katika kupambana na ugaidi na kwamba hatimaye itatoa pigo kubwa na kali kwa magaidi wa kitakfiri wanaojihusisha na vitendo haribifu katika maeneo ya mipaka yake na hata nje ya mipaka hiyo.

Tags