Iran: Usalama hupatikana kwa kupendana si kwa ubeberu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, fikra ya kibeberu na kutumia silaha haribifu inapaswa kuondoka na mahala pake pachukuliwe na fikra ya mazungumzo na kuishi pamoja kwa usalama na kupendana.
Dk Mohammad Javad Zarif alisema hayo Alkhamisi katika kongamano la kimataifa la "Dunia ya Nairuzi (Siku Mpya)" hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa: Mataifa yote ya dunia njooni tutumie lugha ya Iran, lugha ya ardhi ya Nairuzi yaani "siku mpya" na utamamaduni wa Nairuzi; tuseme kwa pamoja kwamba, amani na usalama hauwezi kupatikana kwa kutumia ubeberu na tuwaoneshe walimwengu kwa vitendo na fikra zetu za Kinairuzi kwamba zama za uistikbari na ubeberu zimeisha.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa: Wale watu ambao wametumia dola trilioni saba kuendeshea siasa za kibeberu, hivi sasa hali yao ni mbaya zaidi na hata wakitumia dola trilioni 70 au trilioni 700 hali yao itaendelea kuwa hiyo hiyo.
Matamshi hayo ya Zarif yalikuwa yanailenga Marekani ambayo inatwisha siasa na matakwa yake ya kibeberu katika kona zote za dunia. Moja ya maeneo hayo ni hili la kiistratijia la Asia Magharibi ambapo katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita, Marekani imetumia mabilioni ya dola lakini haijapata chochote isipokuwa kufeli tu na kuendelea machafuko na ukosefu wa usalama katika eneo hili. Serikali ya hivi sasa ya Marekani chini ya urais wa Donald Trump imeongeza kasi kubwa zaidi ya kutekeleza siasa za kibeberu za Marekani za kujikumbizia kila kitu upande wake. Siasa hizo kwa kweli ni hatari kubwa kwa amani na usalama wa dunia nzima na ndio maana jamii ya kimataifa inazipinga vikali.
Kitendo cha serikali ya Trump cha kutoheshimu sheria na mikataba ya kimataifa, na kung'ang'ania kwake kuwauzia silaha waitifaki wake katika maneo tofauti ya dunia likiwemo eneo hili la magharibi mwa Asia kwa ahadi za kuziletea usalama na amani nchi hizo, si tu kwamba zimefeli, lakini pia matokeo yake si mengine ghairi ya kuongezeka machafuko na mauaji katika maeneo hayo.
Ukweli ni kwamba Marekani inazitumia nchi nyingine kujifanikisha malengo yake katika eneo la Asia Magharibi na Ghuba ya Uajemi. Inatumia visingizio vya kuweko vitisho vya kiusalama kuzilazimisha tawala za kiimla kama za Saudi Arabia kujilimbikizia silaha kutoka kwa Marekani. Siasa hizo zimeleta ushindani wa silaha katika eneo hili na licha ya tawala za eneo hili kununua silaha za mabilioni ya dola, lakini zimeshindwa kupata usalama wa kutuliza nyoyo zao. Siasa hizo zilizofeli zinaendelezwa na serikali ya Donald Trump katika hali ambayo licha ya Marekani kutumia fedha nyingi mno, lakini leo hii rais wa nchi hiyo anakwenda katika nchi ya Iraq usiku usiku na kwa kificho. Zaidi ya hayo ni kwamba, licha ya Marekani kuyaunga mkono kila upande magenge ya kigaidi huko Syria, hivi sasa haina chaguo jingine isipokuwa kukimbia nchini humo.
Ni kwa sababu hiyo ndio maana Meja Jenerali Qassem Solaimani, kamanda wa kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH akasema Jumatano usiku kwamba: Marekani imetumia dola trilioni 7 katika eneo hili, lakini pamoja na hayo rais wa nchi hiyo analazimika kwenda Iraq usiku usiku na kwa kujificha.
Uzoefu uliopatikana hivi sasa katika eneo la Asia Magharibi unazidi kuthibitisha ukweli wa matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kwamba silaha na ubeberu hauwezi kuleta usalama na amani na kwamba zama za uistikbari na kutumia mabavu zimeisha.
Njia pekee ya kupatikana amani na utulivu wa kudumu duniani ni hiyo inayosisitizwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yaani kuweko ushirikiano na maelewano ya kuheshimiana na kutoruhusu siasa za kibeberu na kikoloni kukandamiza haki za taifa lolote lile.