Rais Rouhani ataka kushughulikiwa haraka hali ya waathiriwa wa mafuriko Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i52419
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kusisitiza kushughulikiwa haraka hali ya wananchi waliokumbwa na janga la mafuriko katika maeneo mbalimbali hapa nchini amesema kuwa, asasi zote zinapaswa kufanya juhudi maradufu kwa ajili ya kuhakikisha wananchi hao wanafikiwa na misaada haraka iwezekanavyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 26, 2019 15:10 UTC
  • Rais Rouhani ataka kushughulikiwa haraka hali ya waathiriwa wa mafuriko Iran

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kusisitiza kushughulikiwa haraka hali ya wananchi waliokumbwa na janga la mafuriko katika maeneo mbalimbali hapa nchini amesema kuwa, asasi zote zinapaswa kufanya juhudi maradufu kwa ajili ya kuhakikisha wananchi hao wanafikiwa na misaada haraka iwezekanavyo.

Rais Rouhani amesema hayo leo katika kikao cha Idara ya Kukabiliana na Majanga na kulitaka Jeshi na Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH kutumia nyenzo na suhula zote walizonazo kwa ajili ya kuondoa maji katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko.

Reza Ardakanian Waziri wa Nishati wa Iran akizungumza katika kikao hicho amesema kuwa, vijiji 635 katika miji 17 mfumo wake wa maji safi ya kunywa umeharibika kabisa kutokana na janga la mafuriko.

Magari mengi yamesombwa na kuharibiwa vibaya na mafuriko katika mji wa Shiraz, Iran

Hayo yanajiri katika hali ambayo, wananchi wametakiwa kujiepusha na safari zisizo za dharura kwani utabiri wa hali ya hewa unaonyesha kuwa, mvua zingali zinaendelea kunyesha na kuna uwezekano wa kutokea mafuriko katika miji kadhaa hapa nchini.

Kufuatia mvua kubwa ilionyesha katika siku za hivi karibuni, miji kadhaa ya Iran imekumbwa na mafuriko. Hali ya mafuriko ni mbaya zaidi katika miji ya Golestan, Mazandara, Fars na Lorestan.

Jana Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa la Iran lilietahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea mafuriko katika mikoa 12 hapa nchini katika kipindi cha siku tatu zijazo na kuwataka watu kuchuukua tahadhari zaidi.