Iran yataka kuchukuliwe hatua za kukabiliana na waenezaji wa fikra ya ukufurishaji
Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kuchukuliwa msimamo mmoja na madhubuti wa dunia dhidi ya waenezaji wa fikra za ukufurishaji katika maeneo mbalimbali ya ulimwengu.
Es'hagh Al Habib amesema hayo katika hotuba yake kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililokutana kujadili namna ya kutokomeza ubaguzi, chuki dhidi ya wageni na ubaguzi wa rangi ambapo ameashiria matokeo ya shambulio ya kigaidi la hivi karibuni dhidi ya misikiti miwili nchini New Zealand na kusema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani kwa nguvu zake zote hujuma hiyo ya kigaidi na inatoa mkono wa pole kwa familia za wahanga wa shambulio hilo.
Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, matukio kama hayo ya kusikitisha yanaonyesha kuwa, jamii ya kimataifa imeshindwa kukabiliana na malengo ya awali kabisa ya kupambana na ugaidi, ubaguzi, ubaguzi wa rangi na dhulma.
Itakumbukwa kuwa, magaidi wenye chuki za kidini walifanya mashambulizi ya kikatili tarehe 15 Machi mwaka huu katika misikiti miwili mjini Christchurch, nchini New Zealand na kuua shahidi Waislamu 52 waliokuwa katika ibada ya Swala ya Ijumaa na kujeruhiwa makumi ya wengine.
Mmoja wa magaidi waliofanya unyama huo aliandika katika maelezo yake binafsi kwamba, ameathiriwa na fikra za kibaguzi na chuki dhidi ya Waislamu za Rais Donald Trump wa Marekani.