Ayatollah Amoli Larijani: Wananchi wa Iran wanaunga mkono jeshi la SEPAH
Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Iran amelaani vikali hatua ya Marekani dhidi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema kuwa, wananchi wa Iran wanaliunga mkono jeshi hili.
Ayatullah Sadiq Amoli Larijani ameashiria hatua zisizo na hekima na busara za ikulu ya Marekani White House dhidi ya taifa la Iran kwa kuliweka katika orodha ya makundi ya kigaidi Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na kueleza kwamba, hii sio hatua ya kwanza batili ya viongozi wa Marekani.
Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Iran amesema kuwa, hatua ya Marekanii ya kuitangaza Beitul-Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel na vilevile kuutambua rasmi umiliki wa Israel kwa miinuko ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni maghasibu ni mifano mingine ya hatua batili za serikali ya Washington.

Ayatullah Larijani amebainisha kuwa, kitendo kilichoifanya Marekani ichukue hatua ya kukitangaza rasmi kikosi cha nchi fulani ambacho ni sehemu muhimu ya jeshi kuwa ni kundi la kigaidi ni hatua isiyo ya busara, isiyo ya utumiaji akili na ambayo ni kinyume kabisa na sheria za kimataifa.
Siku ya Jumatatu, utawala wa Marekani ulitangaza kuliweka Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika orodha yake ya makundi ya kigaidi.
Kufuatia uhasama huo wa Marekani, Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limetangaza kuwa, wanajeshi wote wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi (CENTCOM) na vikosi vyote vinavyofungamana nao ni kundi la kigaidi.