Waziri Mkuu wa Pakistan kuitembelea Iran, atoa wito wa uhusiano bora
Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan amesema nchi yake inalipa umuhimu mkubwa suala la uhusiano wake na Iran na kuongeza kuwa analenga kuimarisha uhusiano wa nchi hizi mbili jirani katika safari yake tarajiwa mjini Tehran.
Imran Khan ametoa tamko hilo Alhamisi wakati alipokutana na Balozi wa Iran mjini Islamabad Mahdi Honardoost ambapo pande mbili zimejadili safari hiyo.
Akiashiria umuhimu wa safari yake hiyo, Imran Khan amemshukuru Rais Hassan Rouhani wa Iran kwa mwaliko huo ambao amesema utampa fursa ya kuitembelea nchi rafiki na ndugu ya Iran. Aidha ameelezea matumaini yake kuwa, katika safari yake hiyo ya siku mbili, uhusiano wa nchi hizi mbili za Kiislamu utaimarika zaidi.
Waziri Mkuu wa Pakistan anatarajiwa kuwasili nchini Iran Jumapili 21 Aprili ambapo kwanza atafanya ziyara katika Haram ya Imam Ridha AS katika mji mtakatifu wa Mashhad na ziyara hiyo itafanyika katika siku ambayo Waislamu wa madhehebu ya Shia watakuwa wanaadhimisha siku ya kuzaliwa Imam Mahdi, Imamu wa 12 wa Mashia.
Baada ya hapo anatarajiwa kuwasili mjini Tehran kwa lengo la kufanya mazingumzo na viongozi wa ngazi za juu nchini Iran. Imran Khan ambaye alichaguliwa kuwa waziri mkuu wa Pakistan kufuatia ushindi wa chama chake katika uchaguzi mkuu wa Julai 2018 ametangaza kuwa tayari kuwa mpatanishi wa mgogoro uliopo katika uhusiano wa Iran na Saudi Arabia. Mwezi Oktoba mwaka jana Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia Mohammad bin Salman alitembelea Pakistan.