Kama si Iran leo Iraq na Syria zingekuwa zimegawanyika vipande vipande
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i53226-kama_si_iran_leo_iraq_na_syria_zingekuwa_zimegawanyika_vipande_vipande
Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran asema uthabiti na usalama katika eneo umepatikana kwa gharama kubwa na kuongeza kuwa: "Kama si ushirikiano wa kujitolea wa Iran, leo Iraq na Syria zingekuwa zimegawanyika vipande vipande mikononi mwa waovu na maadui wa amani na usalama."
(last modified 2024-06-10T09:25:34+00:00 )
May 02, 2019 07:59 UTC
  • Kama si Iran leo Iraq na Syria zingekuwa zimegawanyika vipande vipande

Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran asema uthabiti na usalama katika eneo umepatikana kwa gharama kubwa na kuongeza kuwa: "Kama si ushirikiano wa kujitolea wa Iran, leo Iraq na Syria zingekuwa zimegawanyika vipande vipande mikononi mwa waovu na maadui wa amani na usalama."

Brigadier General Amir Hatami, Waziri wa Ulinzi wa Iran ameyasema hayo leo Alhamisi mjini Tehran alipokutana na makamanda wa majeshi ya majini na angani ya Jeshi la Iraq. Huku akiashiria hali ya siasa na usalama katika eneo na dunia nzima kwa ujumla amesema: "Iran na Iraq zinakabiliwa na vitisho na fursa na hivyo wakuu wa kisiasa na kijeshi wa nchi mbili wanapaswa kufanya mazungumzo zaidi ili kulinda maslahi ya nchi mbili na kwa ajili ya uthabiti na usalama katika eneo."

Waziri wa Ulinzi wa Iran katika mkutano na makamanda wa Jeshi la Iraq

Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema hatua ya Marekani kulitangaza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kuwa eti ni kundi la kigaidi ilikuwa hatua ya kulipiza kisasi kufuatia hatua ambazo IRGC ilichukua dhidi ya magaidi Syria na Iraq. Amesema lengo jingine la Marekani katika uhasama wake dhidi ya IRGC ni kuvuruga mkondo wa uthabiti wa kisiasa na usalama nchini Iraq na Syria.

Waziri wa Ulinzi wa Iran amebaini kuwa ushirikiano wa Iran na Iraq katika sekta za ulinzi utapelekea kuwepo mlingano, amani, uthabiti na usalama katika eneo.

Wakizungumza katika kikao hicho, makamanda wa kijeshi kutoka Iraq wamesisitiza kuhusu udharura wa kuimarisha uhusiano wa kiulinzi wa nchi mbili.