Iran: Israel ndiyo sababu ya migogoro yote ya kibinadamu Asia Magharibi
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema utawala wa Kizayuni wa Israel ndilo chimbuko la migogoro yote ya kibinadamu katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati).
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeyasema hayo katika taarifa yake kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Nakba, ya kumbukumbu ya mwaka wa 71 tangu kukaliwa kwa mabavu ardhi za Wapalestina.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa, "Miaka 71 iliyopita, utawala wa Kizayuni wa Israel ulizaliwa, utawala ambao hii leo ndiyo asili ya migogoro ya kibinadamu katika eneo la Asia Magharibi. Utawala huo haramu ni tishio kwa usalama na amani ya dunia."
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeeleza bayana kwamba, utawala huo pandikizi unaoendelea kupora ardhi za Wapalestina ulizaliwa kwa uungaji mkono wa Marekani.

Taarifa ya wizara hiyo imesisitiza kuwa, utawala huo haramu umeendelea kuwa hai kwa kuanzisha vita, kutenda jinai na kughusubu ardhi, lakini jamii ya kimataifa ina wajibu wa kusimamisha jinai hizo dhidi ya Wapalestina madhulumu.
Baada ya kughusubiwa ardhi za Palestina mnamo Mei 15 mwaka 1948, Wazayuni walianzisha operesheni ya kuwatimua hatua kwa hatua mamia ya maelefu ya Wapalestina kutoka ardhi zao za jadi, na Wapalestina wanatambua Mei 15 inayosadifiana na tarehe ya kesho kama Siku ya Nakba.