Aug 21, 2019 03:15 UTC
  • Dakta Ali Larijani
    Dakta Ali Larijani

Spika wa Bunge la Iran amesema kuwa Rais Donald Trump wa Marekani amekosea kufananisha medani ya siasa za uwanja wa michezo ya kuigiza na hatua hii inatoa pigo kwa hadhi ya taifa la Marekani.

Akihojiwa na televisheni ya NBC ya Marekani, Dakta Ali Larijani ameashiria mkutano wa Donald Trump na Kiongozi wa Korea Kuskazini Kim Jong-un na kusema kwamba, katika mkutano huo Trump alionekana akimkumbatia Kim Jong-un lakini swali linalojitokeza ni kwamba je, vikwazo vya Washington dhidi ya Korea Kaskazini vimeondolewa? 

Trump na Kim Jong Un

Dakta Larijani pia amezungumzia makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kusema: Vigezo vya Iran katika makubaliano hayo ni vilevile vilivyopo katika makubaliano ya nyuklia. Spika wa Bunge la Iran amesema kuwa, baada ya mazungumzo ya miaka miwili, kulipatikana makubaliano ambayo yalipasishwa kwa azimio la Baraza la Usalama; lakini Wamarekani wamejiondoa katika makubaliano hayo, hivyo wanapaswa kurejea katika fremu iliyoainishwa na jamii ya kimataifa. 

Vilevile ameshiria vitisho vinavyotolewa na Marekani dhidi ya Iran na kusema: Jamhuri ya Kiislamu haijawahi kutaka vita, na hata wakati Wamarekani walipomchochea Saddam Hussein kuianzisha vita dhidi ya Iran haikutaka kuingia vitani. 

Larijani amesisitiza kuwa, vita sio stratijia ya Jamhuri ya Kiislamu lakini iwapo itashambuliwa itajilinda kwa nguvu zote na haitamwacha mchokozi.  

Tags