UN yarefusha muda wa vikosi vya AU kuhudumu Somalia hadi Desemba mwaka huu
(last modified Sat, 17 Aug 2024 09:33:54 GMT )
Aug 17, 2024 09:33 UTC
  • UN yarefusha muda wa vikosi vya AU kuhudumu Somalia hadi Desemba mwaka huu

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha Azimio nambari 2748, linaloruhusu mamlaka ya Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) kusalia nchini humo hadi Desemba mwaka huu.

ATMIS imekuwa ikipunguza uwepo wake nchini Somalia na inatarajiwa kukabidhi majukumu ya usalama kwa vikosi vya nchi hiyo mwishoni mwa mwaka huu.
 
Baada ya azimio hilo kupitishwa, Balozi wa Somalia katika Umoja wa Mataifa, Abukar Dahir Osman alisema, "tunatambua umuhimu wa kurefusha azimio la ATMIS hadi Desemba 2024 ili kuhakikisha kunapatikana mabadiliko mazuri tunapojiandaa kwa ajili ya mpangilio wa usalama wa baada ya ATMIS mwaka 2025. Ni muhimu kujitolea kwa usaidizi unaohitajika kuwezesha Vikosi vya Taifa vya Somalia na ATMIS kuendelea na kazi zao muhimu. Juhudi hizi shirikishi ni muhimu tunapofanya kazi kuelekea kwenye mpito wenye mafanikio kwa ajili ya mfumo mpya wa kulinda amani.”
Abukar Dahir Osman

Hata hivyo Osman amekosoa utekelezwaji wa mchakato wa kupunguza askari wa kulinda amani nchini Somalia na kueleza kwamba, kwa bahati mbaya, kumeshuhudiwa ucheleweshaji katika karibu awamu zote za upunguzaji askari; na akaongeza kuwa ushirikiano mzuri sio tu utawezesha uondoaji salama na kwa utaratibu mzuri wa vikosi vya kulinda amani, lakini pia utapunguza usumbufu unaoweza kutokea wakati wa awamu hiyo hasasi ya kukabidhi mamlaka kamili ya kusimamia usalama kwa vikosi vya nchi hiyo.

 
Azimio jipya la Baraza Usalama limepitishwa miezi kadhaa baada ya Somalia kuutaka Umoja wa Mataifa uhitimishe shughuli za ujumbe wake wa kulinda amani nchini humo kwa ajili ya kupambana na kundi la Al-Shabab lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda.../

 

Tags