Sep 11, 2019 07:35 UTC
  • Iran yatoa mkono wa pole kwa familia za Mashahidi wa Karbala

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetuma salamu za rambirambi kwa serikali ya Iraq na familia za Mashahidi kufuatia tukio la kufa shahidi makumi ya watu katika mji mtakatifu wa Karbala.

Abbas Mousavi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa mkono wa pole kwa serikali na taifa la Iraq kwa ujumla, kufuatia tukio hilo la kuhuzunisha la hapo jana.

Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko pamoja na familia za wahanga wa ajali hiyo. Kadhalika  Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amewaombea saada na ujira wa juu Mashahidi wa tukio hilo, huku akiwatakia afueni ya haraka majeruhi wa tukio hilo.

Wizara ya Afya ya Iraq imetangaza kuwa wafanyaziara 32 wameaga dunia na wengine 108 wamejeruhiwa kutokana na msongamano mkubwa wa watu uliotokea jana katika mlango wa Babul Rajaa ndani ya Haram ya Imam Hussein (as) mjini Karbala. 

Mamilioni ya Mazuwwar mjini Karbala

Maafisa wa usalama wa Iraq wanasema vifo hivyo vimetokana na msongamano mkubwa wa watu katika eneo hilo. 

Zaidi ya Waislamu milioni tatu jana tarehe 10 Muharram ambayo ni maarufu kama Siku ya Ashura, walishiriki katika maombolezo ya kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) katika mji mtakatifu wa Karbala nchini Iraq.

Tags