Salami: Adui hana nguvu yoyote mbele ya taifa la Iran
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema kuwa maadui hawana dira wala nguvu yoyote mkabala wa taifa imara la Iran.
Meja Jenerali Hussein Salami, Kamanda Mkuu wa IRGC amesema hayo katika mkoa wa Ardebil, kaskazini magharibi mwa nchi na kufafanua kuwa, umoja, mshikamano, kusimama kidete na muqawama wa wananchi wa Iran umewafanya maadui wa taifa hili wachanganyikiwe.
Amesisitiza kuwa vikosi vya majeshi ya Iran viko katika kilele cha utayarifu na vitatekeleza amri yoyote kwa kasi ya juu kabisa na kwamba njama za maadui za kuusambaratisha Mfumo wa Kiislamu hapa nchini hii leo zimevurugika kwa kiasi kikubwa kuliko wakati mwingine wowote ule.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza bayana kuwa, "Wanajeshi wa SEPAH katu hawatawaruhusu maadui wajipenyeze katika ardhi ya Iran, na pia wataendelea kuvunja njama za maadui wa taifa hili zinazopikwa maelfu ya kilomita nje ya mipaka ya nchi hii."
Meja Jenerali Hussein Salami ameeleza bayana kuwa "Waliodhani kuwa Iran itasalimu amri mbele ya maadui wamefeli."
Ameashiria kuhusu wimbi la ushindi wa wananchi wa Yemen na kubainisha kuwa, "Wayemen ni wananchi madhulumu, lakini wamesimama kidete na kudumisha muqawama licha ya mashambulizi mtawalia dhidi yao. Mapambano hayo yamepelekea kushindwa maadui licha ya uwezo wao mkubwa."