Bunge la Iran lalaani mashambulizi ya Uturuki dhidi ya Syria
(last modified Mon, 14 Oct 2019 12:08:33 GMT )
Oct 14, 2019 12:08 UTC
  • Bunge la Iran lalaani mashambulizi ya Uturuki dhidi ya Syria

Wawakilishi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) wametoa taarifa wakilaani mashambulizi ya jeshi la Uturuki dhidi ya Syria na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kutetea watu wanaodhulumiwa kote duniani.

Taarifa iliyotolewa leo na wabunge wa Iran imekosoa kimya cha jamii ya kimataifa mbele ya mashambulizi yanayoendelea kufanywa na jeshi la Uturuki huko kaskazini mwa Syria na kusema: Kimya cha nchi zinazodai kutetea haki za binadamu na Umoja wa Mataifa mbele ya mashambulizi hayo kitasajiliwa katika historia. 

Katika taarifa hiyo wabuge wa Iran wametangaza uungaji mkono wao kwa raia Wakurdi wa Syria.

Bunge la Iran

Jumatano iliyopita Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki aliliamuru jeshi la nchi hiyo kufanya mashambulizi dhidi ya eneo la kaskazini mwa Syria kwa kisingizio cha kukabiliana na ugaidi na kuwaangamiza wanamgambo wa Kikurdi katika mpaka wa nchi hizo mbili ambao Ankara inasema wanashirikiana na kundi la wapiganaji wa PKK wanaotaka kujitenga maeneo ya Wakurdi nchini Uturuki. 

Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imelaani vikali mashambulizi na operesheni ya jeshi la Uturuki huko kaskazini mwa nchi hiyo na kuitaja kuwa ni uvamizi dhidi ya ardhi ya Syria.