Zarif: Ulaya imeshindwa kutekeleza majukumu yake ndani ya JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i56667-zarif_ulaya_imeshindwa_kutekeleza_majukumu_yake_ndani_ya_jcpoa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Ulaya imeshindwa kutekeleza majukumu yake ndani ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na iwapo pande husika katika makubaliano hayo hazitayatekeleza, Iran itachukua hatua za dharura za kupunguza utekelezaji wa mapatano hayo ya nyuklia.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Oct 16, 2019 22:09 UTC
  • Zarif: Ulaya imeshindwa kutekeleza majukumu yake ndani ya JCPOA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Ulaya imeshindwa kutekeleza majukumu yake ndani ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na iwapo pande husika katika makubaliano hayo hazitayatekeleza, Iran itachukua hatua za dharura za kupunguza utekelezaji wa mapatano hayo ya nyuklia.

Dakta Muhammad Javad Zarif ameyasema hayo katika kikao cha Kamisheni ya Pamoja ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Afrika ya Kusini kilichohudhuriwa pia na waziri mwenzake Naledi Pandor mjini Tehran. Amesema kuwa kujiondoa kwa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kumekiuka waziwazi azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na ni kinyume na matakwa na maamuzi ya wanachama wote wa umoja huo. 

Zarif amesema kuwa, Iran ilitekeleza majukumu yake yote katika makubaliano ya nyuklia hadi Marekani ilipojiondoa na kuongeza kuwa: Tehran imesitisha kisheria utekelezaji wa baadhi ya vipengee vya makubaliano hayo kwa mujibu wa vipengee nambari 26 na 36 vya JCPOA. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu na Afrika Kusini zina mitazamo inayofanana katika masuala mengi ya kikanda na kimataifa na kuongeza kuwa: Kuna udharura wa kuimarishwa zaidi uhusiano wa kiuchumi, kibiashara, kiufundi na kisayansi wa nchi hizi mbili kwa kushirikisha sekta za serikali na za watu binafsi. 

Iran na Afrika Kusini zimesaini hati kadhaa za ushirikiano

Kwa upande wake Waziri wa Mahusiano na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Naledi Pandor amekumbusha misaada yenye thamani kubwa ya Iran kwa mapambano ya kupigania uhuru ya watu wa Afrika kusini dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Apartheid na kusisitiza upinzani wa nchi yake dhidi ya sera a kujichukua maamuzi ya upande mmoja na udharura wa kudumishwa ushirikiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kielimu na katika masuala ya nishati.

Pande hizo mbili pia zimesaini hati za ushirikiano wa kimataifa na kusisitiza udharura wa kudumishwa ushirikiano wa nchi mbili kupitia Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM), kupambana na ugaidi na kendelezwa mashauriano na jitihada za kidiplomasia za kuimarisha amani na usalama duniani.