Zoezi la kujiandikisha wanaotaka kugombea ubunge Iran laanza
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i57621-zoezi_la_kujiandikisha_wanaotaka_kugombea_ubunge_iran_laanza
Zoezi la uandikishaji wagombea wa uchaguzi wa awamu ya 11 Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, limeanza rasmi Jumapili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 02, 2019 01:10 UTC
  • Zoezi la kujiandikisha wanaotaka kugombea ubunge Iran laanza

Zoezi la uandikishaji wagombea wa uchaguzi wa awamu ya 11 Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, limeanza rasmi Jumapili.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran Abdul Ridha Rahmani Fazli alizindua zoezi hilo la uandikishaji  wawale wanaotaka kugombea ubunge ambapo mbali na kujiandikisha katika Makao Makuu ya Uchaguzi mjini Tehran, pia wanaweza kujiandikisha katika ofisi za wakuu wa mikoa kote nchini.

Wanaokusudia kushiriki katika uchaguzi wa Bunge la Iran wana hadi 7 Disemba kujiandikisha.

Baada ya kujiandikisha, majina yao yatapelekwa katika Idara ya Mahakama, Idara ya Polisi, Wizara ya Usalama na Idara ya Usajili wa Watu na idara hizo zitakuwa na muda wa siku tano kubaini iwapo waliojisajili wanaweza kuwania ubunge au la. Baada ya hapo Baraza la Kulinda Katiba nalo litakuwa na muhula wa hadi Februrari 11 2020 ili kuchunguza iwapo waliojinadikisha wametimiza masharti yote ya kugombea ubunge.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran Abdul Ridha Rahmani Fazli akiwasili katika Makao Makuu ya Uchaguzi

Baaada ya kumalizika mchakato huo, Makao Makuu ya Uchaguzi katika Wizara ya Mambo ya Ndani yatatoa tangazo la kuanza rasmi kampeni za uchaguzi Februari 13. Uchaguzi wa Bunge la Iran umepangwa kufanyika Februari 21 katika maeneo bunge 208 kote Iran kwa ajili ya kuwachagua wabunge 290.

Aidha katika siku hiyo pia kutafanyika uchaguzi mdogo wa baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Muadhamu katika majimbo ya Tehran, Fars, Khorassan Kaskazini, Khorassan Ravazi na Qum.