Iran yasitisha utekelezaji wa makubaliano ya JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i58338-iran_yasitisha_utekelezaji_wa_makubaliano_ya_jcpoa
Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran usiku wa kuamkia leo Jumatatu imetoa taarifa ikitangaza kuwa imechukua hatua ya tano na ya mwisho ya kupunguza utekelezaji wa ahadi zake katika makubaliano ya nyuklia maarufu kwa kifupi kama JCPOA.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 06, 2020 00:08 UTC
  • Iran yasitisha utekelezaji wa makubaliano ya JCPOA

Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran usiku wa kuamkia leo Jumatatu imetoa taarifa ikitangaza kuwa imechukua hatua ya tano na ya mwisho ya kupunguza utekelezaji wa ahadi zake katika makubaliano ya nyuklia maarufu kwa kifupi kama JCPOA.

Taarifa hiyo imesema kuwa, kuanzia sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitakuwa na kizuizi chochote katika shughuli zake za nyuklia ikiwa ni pamoja na kurutubisha madini ya urani, asilimia ya urutubishaji wa madini hayo, kiwango kinachorutubishwa na katika masuala ya utafiti na uchunguzi. 

Kwa msingi huo katika hatua hii ya tano, Jamhuri ya Kiislamu imetupilia mbali kizuizi muhimu zaidi cha shughuli zake kwa mujibu wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ambacho kinahusiana na idadi ya mashinepewa zinazoruhusiwa kufanya kazi. 

Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema katika taarifa hiyo kwamba, tokea sasa miradi yake ya kuzalisha nishati ya nyuklia itafanya kazi kwa mujibu wa mahitaji yake ya kiufundi. Imesisitiza kuwa, Iran itaendelea kushirikiana na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na kwamba iwapo vikwazo vyote vitaondolewa na Tehran ikafaidika na maslahi ya JCPOA, Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kutekeleza tena vipengee vya makubaliano hayo. 

Miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran

Baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano hayo ya kimataifa mwezi Mei 2018 nchi za Ujerumani, Uingereza na Ufaransa ziliahidi kwamba zitadhamini maslahi ya kiuchumi ya Iran kwa mujibu wa mapatano hayo. Hata hivyo zimeshindwa kutekeleza ahadi zao licha ya kuilaani hatua ya Marekani ya kujiondoa katika JCPOA. 

Iran ilianza kusitisha utekelezaji wa vipengee vya mapatano hayo baada ya Marekani kujiondoa na nchi za Ulaya kushindwa kutekeleza majukumu yao. 

Kwa mujibu wa vingee vya 26 na 36 vya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Iran ina haki ya kusitisha baadhi au vipengee vyote vya makubaliano hayo iwapo upande wa pili hautaheshimu na kutekeleza majukumu yake.