UN katika mzingiro wa ukwamishaji wa Marekani; Washington yakataa kumpa viza Zarif
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i58443-un_katika_mzingiro_wa_ukwamishaji_wa_marekani_washington_yakataa_kumpa_viza_zarif
Majid Takhte Ravanchi, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amemuandikia barua Katibu Mkuu wa umoja huo na kubainisha malalamiko makali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ukwamishaji wa serikali ya Trump wa kutompa viza Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kwa ajili ya kushiriki katika kikao cha Baraza la Usalama.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 11, 2020 08:03 UTC
  • UN katika mzingiro wa ukwamishaji wa Marekani; Washington yakataa kumpa viza Zarif

Majid Takhte Ravanchi, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amemuandikia barua Katibu Mkuu wa umoja huo na kubainisha malalamiko makali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ukwamishaji wa serikali ya Trump wa kutompa viza Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kwa ajili ya kushiriki katika kikao cha Baraza la Usalama.

Katika barua aliyoituma jana kwa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Majid Takhte Ravanchi alieleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu hatua ya Marekani ya kukariri kutoheshimu wadhifa wa kisheria na kustafidi na nafasi yake ya kuwa mwenyeji wa makao makuu ya umoja huo huko New York kama wenzo wa kisiasa dhidi ya nchi nyingine. 

Takhte Ravanchi, amemtaka Katiba Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuipatia ufumbuzi changamoto hiyo kwa mujibu wa kipengee cha 21 cha hati ya makao makuu hayo ya Umoja wa Mataifa ambayo yanahoji itibari ya muundo wa umoja huo.  

Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu alitazamia kuelekea New York siku ya Alkhamisi iliyopita kwa ajili ya kushiriki kikao cha Baraza la Usalama katika ngazi ya Mawaziri wa Mambo ya Nje. Hata hivyo katika kuendeleza mashinikizo yake ya juu zaidi dhidi ya Iran, serikali ya Marekani imekataa kumpa viza mkuu huyo wa chombo cha diplomasia wa Iran kwa ajili ya safari hiyo ya New York. 

Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran 

Kitendo cha Marekani cha kutumia kama wenzo na kinyume cha sheria nafasi ya nchi hiyo ya kuwa mwenyeji wa makao makuu ya Umoja wa Mataifa kinaathiri shughuli za umoja huo. Kwa mujibu wa kanuni na misingi ya awali ya taasisi hiyo ya kimataifa; serikali ya Marekani inapasa bila ya kizingizio chochote kuzipatia kibali cha kuingia nchini humo wanachama wote wa Umoja wa Mataifa; na Wizara ya Mashauri ya Kigeni na hata taasisi za usalama za nchi hiyo hazina haki ya kukwamisha au hata kubainisha mitazamo yao kuhusu wawakilishi wa nchi wanachama na wale wanaoshiriki kwenye mikutano mbalimbali. 

Kuhusiana na suala hilo, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limewasilisha maazimio mengi ambayo yanazizuia serikali kutekeleza vizuizi na sheria za ziada dhidi ya nchi nyingine. Kipengee cha 2 cha kifungu cha 7 cha hati ya Umoja wa Mataifa kinaweka wazi kanuni za kupiga marufuku nchi wanachama wa umoja huo kuingiliana katika masuala yao ya ndani.

Kabla ya hili pia, mwezi  Septemba mwaka jana, Marekani ilikwamisha safari ya Zarif ya kuelekea New York wakati wa vikao vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa; na ilichelewesha kuupatia ujumbe wa Iran viza za kuingia Marekani. 

Aidha mwezi Julai mwaka jana serikali ya Marekani ilimuwekea vizuizi vikubwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran wakati wa safari yake mjini New York kwa ajili ya kushiriki kikao cha ngazi ya juu cha Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa. 

Moja ya ahadi ilizotoa Marekani kwa mujibu wa makubaliano ya mwaka 1947 ya kuweko nchini humo makao makuu ya Umoja wa Mataifa ni kuwa, inalazimika kuheshimu misingi ya kidiplomasia na kuwalinda wajumbe wa kidiplomasia wa nchi wanachama wa umoja huo na vile vile kutowakwamisha wajumbe wa nchi wanachama kushiriki mikutano na vikao vya Umoja wa Mataifa huko New York. 

Hata hivyo kutangazwa kumuwekea vizuizi Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu katika safari zake za kikazi huko New York ni jambo lililotazamiwa sana hasa kutokana na vitendo vya ajabu ajabu vya viongozi wa Marekani.  

Tangu ashike hatamu za urais huko White House, Donald Trump amekiuka mara nyingi sheria na kanuni za kimataifa na kuifanya jamii ya kimataifa ikabiliwe na changamoto chungu nzima. Nukta ya kuzingatia hapa kuhusiana na suala hilo nyeti ni kwamba Mike Pompeo Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani Julai 14 mwaka jana alikiri mwenyewe katika mahojiano na gazeti la Washington Post kuwa: Ana wasiwasi na taathira za safari za kikazi za Zarif na namna safari hizo zitakavyoziathiri fikra za waliowengi huko Marekani na ulimwenguni kwa ujumla.  

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, Mike Pompeo 

Marekani kwa kutumia tajiriba ya mbinu za safari za huko nyuma za Zarif na uwoga ilio nao kuhusu taathira ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kwa siasa za ndani za Marekani hususan katika kipindi cha hivi sasa, inafanya kila iwezalo kuwawekea vizuizi na kukwamisha safari za kidiplomasia za viongozi wa Iran ili kuzuia tatahira za nguvu laini za Iran kwa fikra za walio wengi huko Marekani na ulimwenguni kwa ujumla.