Rais Rouhani: Muamala wa Karne ni mpango muovu kabisa wa karne
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran usiku wa kuamkia leo amesema kuwa, mpango wa Marekani wa Muamala wa Karne ni mpango muovu kabisa wa karne.
Rais Hassan Rouhani ameandika hayo kwa lunga ya Kiingereza kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kusema kuwa, hatua hizo za kijinga zinachosha, huu ni mpango muovu kabisa wa karne.
Kwa upande wake, Dk Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, jana usiku alisema, mpango wa Muamala wa Karne wa Kimarekani-Kizayuni ni barabara kubwa na pana ya kuelekea motoni.
Juzi Jumanne, rais wa Marekani Donald Trump akiwa pamoja na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alizindua rasmi mpango wake wa kibaguzi aliouita eti Muamala wa Karne.
Mpango huo unakanyaga kikamilifu haki za Wapalestina lakini cha kusikitisha zaidi ni kuona kuwa baadhi ya nchi za Kiarabu kama vile Saudi Arabia, Bahrain, Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu zinashirikiana kikamilifu ya Marekani katika njama hizo.
Kwa mujibu wa njama hizo mpya za Marekani, mji mzima wa Baytul Muqaddas utakabidhiwa kwa utawala wa Kizayuni na wakimbizi wa Palestina hawatokuwa na haki ya aina yoyote ya kurejea kwenye ardhi za mababu zao. Makundi yote ya Palestina yamelaani vikali njama hizo.
Nchi nyingi duniani, watu maarufu, vyama, taasisi na makundi ya kisiasa na kidini hususan ya Waislamu yanaendelea kulaani vikali mpango huo ambao umepewa jina la muamala muovu zaidi wa karne.