Iran yapinga azimio la Bodi ya Magavana ya IAEA
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa hatua ya Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuandamana na Marekani katika azimio dhidi ya Iran ambalo limepasishwa katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).
Katika ujumbe kupitia ukurasa wake wa Twitter Ijumaa usiku, Mohammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amezikosoa nchi hizyo tatu kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao katika mapatano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA). Aidha amesema nchi hizo tatu zimefuata nyayo za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel katika kuipinga Iran. Zarif pia amesema nchi hizo tatu za Ulaya hazina hadhi ya kuinasihi Iran.
Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki Ijumaa ilipitisha azimio ambalo limependekezwa na Troika ya Ulaya yaani Ujerumani, Uingereza na Ufaransa, dhidi ya Iran pamoja na kuwa azimio hilo limepingwa na China na Russia.
Naye Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa tamko baada ya Bodi ya Magavana ya IAEA kupasisha azimio lililopendekezwa na nchi tatu za Ulaya dhidi ya Iran na kusema halikubaliki na ni la kisiasa.
Katika taarifa Ijumaa usiku Sayyid Abbas Mousavi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema azimio hilo la IAEA si la uwajibikaji na halikubaliki.
Akipinga kikamilifu azimio hilo, Mousavi amelitaja kuwa lisilo la kitaalamu na kuongeza kuwa: “Katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inashirikiana kwa kiwango cha juu zaidi na IAEA, kupasishwa azimio kama hilo ni jambo la kusikitisha.”
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema IAEA imekuza kupita kiasi maombi ya baadhi ya nchi zikiongozwa na Marekani na kwamba kinachoshuhudiwa ni njama za kuibua mgogoro mpya kuhusu ushirikiano wa Iran na IAEA.

Mousavi amewataka wanachama wa Bodi ya Magavana ya IAEA kuwa macho mbele ya njama za Marekani na utawala wa Kizayuni za kufungua mafaili bandia ya zamani yasiyo na mashiko na ambayo yalibainika kuwa yasiyo na msingi na yakafungwa na bodi hiyo ya magavana.
Aidha amezishukuru nchi ambazo zimetambua malengo ya kisiasa yaliyo nyuma ya pazia la azimio hilo na hivyo kukataa kuliunga mkono. Mousavi pia amesema nchi ambazo zimeunga mkono azimio hilo zingepaswa kufahamu kuwa Marekani na utawala wa Kizayuni zina malengo fiche ya kuibua mgogoro mpya wa kimataifa. Aidha Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amezilaani vikali Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kwa kuarifisha azimio hilo chini ya mashinikizo ya Marekani. Amesema nchi hizo tatu zimeshindwa kutekelezwa majukumu yao katika mapatano ya JCPOA na hivyo kuwasilisha azimio hilo ni njia ya kukwepa majukumu yao ya JCPOA mbele ya Iran.