Marekani ya Trump; utawala asi na wa kijambazi duniani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i62381-marekani_ya_trump_utawala_asi_na_wa_kijambazi_duniani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, baada ya Marekani kujitoa katika makubaliano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) imegeuka kuwa utawala asi na wa kijambazi duniani.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Jul 23, 2020 22:12 UTC
  • Marekani ya Trump; utawala asi na wa kijambazi duniani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, baada ya Marekani kujitoa katika makubaliano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) imegeuka kuwa utawala asi na wa kijambazi duniani.

Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Sputnik la Russia wakati akichambua sera za Marekani baada ya kujitoa katika JCPOA na akaeleza kuwa, ni hakika kwamba Mareani imegeuka kuwa utawala asi na mvunjaji sheria; na jamii ya kimataifa imefikia natija kuwa Marekani si mshirika wa kumtegemea.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif

Baada ya Donald Trump kuingia Ikulu ya White House, dharau na upuuzaji wa sheria na makubaliano ya kimataifa pamoja na kuachana na mtazamo wa uchukuaji maamuzi ya pamoja kwa makubaliano ya pande kadhaa, ulikuwa ndio mwenendo rasmi uliofuatwa na Marekani ya Trump.

Kwa kufuata muelekeo wa kujifanyia mambo kivyake sambamba na kukiuka sheria na taratibu za kimataifa, mbali na Trump kujiondoa katika JCPOA, alijitoa pia katika mashirika na makubaliano ya kimataifa moja baada ya jengine. Igizo la karibuni kabisa la onyesho hilo la Trump katika uga wa kimataifa ni kujitoa Marekani katika Shirika la Afya Duniani WHO wakati huu ambapo dunia nzima inataabika katika kupambana na janga la ulimwengu mzima la ugonjwa wa Covid-19.

Wamarekani waliowengi wamechoshwa na Trump

Mwenendo ilioamua kufuata Marekani hivi sasa ni hatari kwa utawala wa sheria na mfumo wa uchukuaji hatua kwa makubaliano ya pande kadhaa; na kwa hakika tabia ya Marekani ya Trump ni hatarishi kwa maslahi ya jamii ya kimataifa na hata kwa Wamarekani wenyewe.

Nchi inayovunja kanuni na taratibu za kimataifa na isiyoheshimu ahadi na majukumu iliyojikubalisha, haistahili jina jengine isipokuwa kuitwa utawala asi na wa kijambazi; na kuendelea kwa mwenendo huo hakuna tija yoyote kwa mfumo wa kimataifa isipokuwa kuzidi kushamirisha ukosefu wa amani duniani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif anaitakidi kuwa, jambo linalohitajiwa leo hii na mfumo wa kimataifa ni kujikita na kutilia mkazo utawala wa sheria na uchukuaji maamuzi ya pamoja ya kambi za pande kadhaa ili kudhamini maslahi ya nchi zote.

Kwa kutoa mfano, katika kipindi hiki cha janga la dunia nzima la maradhi ya Covid-19, kinachoweza kudhamini usalama wa afya za wanadamu wote na kukabiliana na virusi visivyojali mipaka ya kijiografia vya maradhi hayo, ni ushirikiano wa pamoja wa kifikra na wa uchukuaji hatua na utumiaji wa tajiriba za utabibu na utengezaji wa dawa wa nchi mbali mbali duniani. Mhimili mkuu wa kuratibu mashirikiano hayo ya pamoja katika kupambana na ugonjwa wa corona ni Shirika la Afya Duniani WHO, ambalo jukumu lake muhimu zaidi ni kuyalinda maisha ya watu na tishio la maradhi mbalimbali.

Katika hali na mazingira kama haya, ukiukaji wa taratibu na uvunjaji sheria uliofanywa na Marekani wa kujitoa katika WHO, si kwa manufaa ya jamii ya kimataifa, walimwengu au hata wananchi wa Marekani, bali kuna madhara kwa juhudi za kimataifa za kukabiliana na janga la corona na kulinda siha na afya za walimwengu wote.

Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi anaamini kuwa, wakati maisha ya mamilioni ya watu yako hatarini kutokana na maradhi angamizi ya corona, Donald Trump anazorotesha na kudumaza jitihada zinazofanywa kimataifa ili kuyashinda na kuyatokomeza maradhi hayo.

Shahid kamanda Qassem Soleimani

Mauaji ya kigaidi ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa kamanda wa kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) yaliyofanywa ndani ya ardhi ya Iraq ni kielelezo cha upeo wa jeuri na ushenzi wa utawala wa Marekani kutokana na kujusuru kumuua kigaidi mgeni rasmi wa Wairaqi na jemadari halisi wa mapambano dhidi ya ugaidi katika eneo la Asia Magharibi.

Kujitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na mashirika ya kimataifa na muhimu zaidi ya yote kudharau kanuni na sheria za kimataifa na vile vile kukiri hadharani kuwa imemuua kigaidi kamanda Qassem Soleimani, ni ushahidi wa wazi unaothibitisha kuwa Marekani ya Trump imegeuka kuwa utawala asi na wa kijambazi ambao hautakuwa na matokeo mengine isipokuwa kueneza wimbi la uvunjaji sheria na uvurugaji amani na usalama duniani kote.../