Aug 25, 2020 08:06 UTC
  • Zarif aushangaa uchu wa Pompeo wa kurundika silaha za US Asia Magharibi

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemkosoa vikali Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani kwa kuvunja sheria za nchi hiyo ili kukidhi uchu wake wa kutaka kuuza silaha za kijeshi kwa wingi katika nchi za eneo la Asia Magharibi.

Katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Mohammad Javad Zarif amemhutubu Mike Pompeo kwa kusema: Huku akiwa amesimama kando ya tishio nambari moja la (silaha za) nyuklia duniani, (Pompeo) ametangaza wazi uchu wake wa kurundika silaha zaidi za Marekani katika eneo, katika hali ambayo anajaribu kuzuia kufanywa wa kawaida ushirikiano halali wa kiulinzi wa Iran na dunia.

Awali gazeti la Marekani la New York Times liliripoti kuwa, utawala wa Rais Donald Trump unakanyaga Sheria ya Kudhibiti Silaha na kuuuzia Umoja wa Falme za Kiarabu ndege zisizo na rubani na zilizosheheni silaha na ndege za kivita aina ya F-35.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, hatua hiyo imepingwa vikali ndani ya Marekani na maafisa wa kudhibiti mauzo ya silaha pamoja na wabunge wanaojaribu kuzuia ueneaji wa silaha za namna hiyo duniani, hususan kwa nchi kama Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Waziri Zarif

Akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu mjini Quds (Jerusalem) hapo jana, Pompeo alisema Marekani ina uhusiano wa kijeshi wa zaidi ya miaka 20 na Imarati, na kwamba itaendelea kuiuzia silaha kwa wingi nchi hiyo ya Kiarabu.

Haya yanajiri siku chache baada ya Abu Dhabi na Tel Aviv kusaini mkataba na kuafikiana rasmi kuanzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia, chini ya kile kilichotajwa kama upatanishi wa Marekani; makubaliano ambayo yamekabiliwa na wimbi kali la malalamiko na upinzani wa makundi ya Palestina, nchi za Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi na shakhsia kadhaa wa kisiasa, kijamii na kidini kote duniani.

Tags