Araqchi: Vita vitaisha kwa njia itakayomfanya adui asifikirie tena kutushambulia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137422-araqchi_vita_vitaisha_kwa_njia_itakayomfanya_adui_asifikirie_tena_kutushambulia
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu haijatuma ujumbe wa aina yoyote kwa wavamizi wala haijaomba kusitishwa vita.
(last modified 2026-03-17T07:01:04+00:00 )
Mar 17, 2026 07:01 UTC
  • Sayyid Abbas Araqchi
    Sayyid Abbas Araqchi

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu haijatuma ujumbe wa aina yoyote kwa wavamizi wala haijaomba kusitishwa vita.

Sayyid Abbas Araqchi amesema: Mwanoni mwa mwaka huu tulikuwa na vita vilivyoanzishwa na maadui wa Iran kwa wito wa kuitaka Tehran ijisalimishe bila ya masharti yoyote; na baada ya siku 12 maadui waliomba kusitishwa mapigano. Mara hii pia wamefanya hivyo hivyo tena kwa nguvu kubwa zaidi ili kuilazimisha Iran kusalimu amri bila masharti yoyote.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: Hivi sasa, baada ya kupita zaidi ya siku 15 za vita, adui anaziomba nchi nyingine ziingilie kati kwa ajili ya usalama wa Lango Bahari la Hormuz ili lango hilo lifunguliwe tena. “Tumo katika mapambano ya kutia fahari na tunaendeleza muqawama bila kuyumba,” amesema Araqchi.

Amesisitiza kuwa: “Iran haijatuma ujumbe wa aina yoyote kwa wavamizi wala haijaomba kusitishwa mapigano. Lakini vita hivi vinapaswa kumalizika kwa njia ambayo havitarudiwa tena, na adui asifikie tena kufanya uchokozi wake. Hadi sasa pia maadui wa Iran wamepewa somo zuri.”

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza: Sasa, maadui wametambua wanakabiliana na taifa la aina gani; hatuna wasiwasi kuhusu nguvu zetu za kujilinda na tutaendeleza vita kadiri inavyohitajika.