Zarif: Tunataka tuwe na uhusiano mzuri na IAEA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i63032-zarif_tunataka_tuwe_na_uhusiano_mzuri_na_iaea
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba ziara ya Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA hapa nchini ilikuwa na mafanikio makubwa na kusisitiza kuwa, Tehran inataka kuwa na uhusiano wa kawaida na mzuri na wakala huo na kuonya kuhusu ukwamishaji mambo unaofanywa na maadui.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 26, 2020 03:17 UTC
  • Zarif: Tunataka tuwe na uhusiano mzuri na IAEA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba ziara ya Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA hapa nchini ilikuwa na mafanikio makubwa na kusisitiza kuwa, Tehran inataka kuwa na uhusiano wa kawaida na mzuri na wakala huo na kuonya kuhusu ukwamishaji mambo unaofanywa na maadui.

Dk Mohammad Javad Zarif aidha ameandika: Iran muda wote imekuwa ikifanya mambo yake kwa uwazi kabisa na kwamba zaidi ya asilimia 92 ya ukaguzi wa maafisa wa IAEA umefanyika nchini Iran. 

Aidha ameonya kwa kusema, kuna baadhi ya watu wanajaribu kukwamisha uwazi huo kupitia mashinikizo na kufufua mafaili yashayofungwa.

Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA aliwasili hapa Iran juzi Jumatatu akiongoza ujumbe wa wakala huo kwa ajili ya ziara rasmi ya siku mbili ambapo ameonana na viongozi mbalimbali wa Iran.

Jana Jumanne alionana na Dk Ali Akbar Salehi, Mkuu wa Taasisi ya Nyuklia ya Iran (AEOI) na kufanya mazungumzo yaliyofana.

Katika mazungumzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA alikiri kwamba wakala huo uko chini ya mashinikizo lakini vile vile alisisitiza kuwa kamwe hatoruhusu mashinikizo hayo yaathiri kazi za IAEA.

Amma kuhusiana na mradi wa nyuklia ya Saudi Arabia, Mkurugenzi Mkuu huyo wa IAEA amesema, imeamuliwa kwamba shughuli za nyuklia za Saudi Arabia ziwekwe chini ya uangalizi wa wakala huo.