Khatibzadeh: Si muhimu ni nani anakuwa rais wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i63200-khatibzadeh_si_muhimu_ni_nani_anakuwa_rais_wa_marekani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa hakuna umuhimu kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba ni nani anakuwa rais wa Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 03, 2020 06:44 UTC
  • Khatibzadeh: Si muhimu ni nani anakuwa rais wa Marekani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa hakuna umuhimu kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba ni nani anakuwa rais wa Marekani.

Saeed Khatibzadeh ameongeza kuwa, viongozi wa Marekani wamezoea kuanzisha kampeni dhidi ya usalama wa baadhi ya nchi nyingine. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameyasema haya akijibu matamshi ya Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa ya Marekani kwamba Iran inaingilia uchaguzi wa nchi hiyo. Khatibzadeh amesema kuwa, kwa hakika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haishughulishwi kivyovyote na siasa za ndani ya Marekani. Amesema kinachotokea ndani ya Marekani kinawahusu Wamarekani wenyewe. 

John Ratcliffe, Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa ya Marekani 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa: kadhia muhimu kwa Iran ni Marekani iheshimu ahadi na majukumu yake ya kimataifa; iache uasi na vitendo vya kipumbavu. Amesema kuwa, suala lililo na umuhimu kuliko yote ni kwamba Marekani iheshimu haki ya taifa la Iran na kufidia hasara zote ilizoisababishia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

John Ratcliffe Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa ya Marekani siku chache zilizopita alidai kuwa, eti Iran, Russia na China zinajaribu kuingilia uchaguzi wa Marekani. 

Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa ya Marekani aliongeza kuwa China, Russia na Iran na pande nyingine zinafanya juhudi za kuingilia au kuathiri uchaguzi wa Marekani kwa malengo yao.