Iran: Marekani ni kidhabi kwa kudai vikwazo vipya havilengi sekta ya afya
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i63958-iran_marekani_ni_kidhabi_kwa_kudai_vikwazo_vipya_havilengi_sekta_ya_afya
Waziri wa Afya wa Iran amelaani hatua ya Marekani ya kuliwekea vikwazo shadidi taifa hili na kubainisha kuwa, utawala wa Washington umekubuhu kwa kusema uwongo, kwa madai yake kuwa vikwazo vipya dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu havilengi sekta ya afya na tiba.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 11, 2020 08:41 UTC
  • Iran: Marekani ni kidhabi kwa kudai vikwazo vipya havilengi sekta ya afya

Waziri wa Afya wa Iran amelaani hatua ya Marekani ya kuliwekea vikwazo shadidi taifa hili na kubainisha kuwa, utawala wa Washington umekubuhu kwa kusema uwongo, kwa madai yake kuwa vikwazo vipya dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu havilengi sekta ya afya na tiba.

Saeed Namaki amesema hayo leo Jumapili na kuongeza kuwa, Marekani inadanganya wazi wazi kwa kudai kuwa sekta ya dawa na tiba haijalengwa katika vikwazo vipya ilivyotangaza siku chache zilizopita dhidi ya wananchi wa Iran.

Ameeleza bayana kuwa, utawala wa sasa wa Marekani unaoongozwa na Donald Trump ndio mbaya zaidi na wenye uhasama mkubwa zaidi kwa taifa la Iran katika historia.

Hata hivyo Waziri wa Afya wa Iran amesisitiza kuwa, licha ya mashinikizo na vikwazo hivyo vya kikatili na kidhalimu vya Marekani, lakini nchi hii haikabiliwi na uhaba wa dawa.

Dawa ya kukabiliana na virusi ya 'Remdesivir' iliyozalishwa Iran

Namaki amefafanua kwa kusema: Iran imeweza kuzalisha dawa aina ya 'Remdesivir' na 'Favipiravir' na hivi karibuni zitaanza kuuzwa nje ya nchi. Dawa hizi zinatumika katika nchi mbali mbali duniani kupunguza makali ya virusi vya corona.

Kuhusu uzalishaji wa chanjo ya ugonjwa wa Covid-19, Dakta Namaki amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaitangazia dunia habari njema juu ya chanjo hiyo ndani ya wiki chache zijazo.