Ghalibaf: Kasi ya kuporomoka Marekani imeongezeka
(last modified Sun, 15 Nov 2020 08:12:40 GMT )
Nov 15, 2020 08:12 UTC
  • Ghalibaf: Kasi ya kuporomoka Marekani imeongezeka

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, matukio yaliyoambatana na uchaguzi wa Marekani yamezidi kuporomosha itibari ya nchi hiyo na kuongeza kasi ya kuporomoka mfumo wa kibeberu wa Marekani.

Mohammad Bagher Ghalibaf amesema hayo leo asubuhi na kuongeza kuwa, matatizo ya kimuundo, kijamii, kisiasa na kiuchumi ya Marekani yamejionesha kwa uwazi kabisa mbele ya walimwengu baada ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo na kwamba taswira halisi ya hivi sasa inaonesha kuongezeka kasi ya kuporomoka Marekani na kuvunjika nguvu dola hilo la kibeberu mbele ya macho ya wanyonge ulimwenguni. Spika wa Bunge la Iran amegusia uhakika mwingine kwamba, kubadilishwa sura za watu katika uongozi wa Marekani hakubadilishi chochote katika siasa za tawala za Marekani kuhusu Iran na kuongeza kwamba, lililo muhimu kwa Iran ni hatua za kivitendo za serikali ya Joe Biden na kuna wajibu wa kuona mauzo ya mafuta ya Iran, mabadilishano yake ya kibenki na biashara za mashirika ya Iran na dunia zinarejeshwa kwenye hali yake ya kawaida katika serikali ijayo ya Marekani.

Trump na Biden

 

Vile vile amesema, ripoti za mara kwa mara za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki zimethibitisha kwamba Iran imeheshimu kikamilifu ahadi zake za nyuklia na kuongeza kwamba, kama kweli Joe Biden ana imani na mapatano ya nyuklia ya JCPOA, basi hana budi ila kutekeleza ahadi za Marekani kwenye makubaliano hayo bila ya kuweka masharti yoyote na pia iwalipe fidia wananchi wa Iran kwa kushindwa Marekani kutekeleza ahadi zake ndani ya JCPOA, kwa miaka kadhaa sasa. Spika Qalibaf amesisitiza kwamba Iran inaamini kuwa mfumo uliooza wa Marekani ndio hasa wa kulaumiwa kutokana na maamuzi ghalati yanayochukuliwa na viongozi wa nchi hiyo. Amesema, kisasi pekee cha kufidiwa damu za mashahid Qassem Soleimani na Abu Mahdi al Muhandis ni kutimuliwa wanajeshi wa Marekani katika eneo hili.