Rais Rouhani: Vikwazo vya kidhulma dhidi ya Iran lazima vifutwe
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, vikwazo vya kidhulma dhidi ya Iran lazima vifutwe.
Rais Hassan Rouhani amesema hayo leo Jumatatu mbele ya waandishi wa habari wa ndani na nje ya Iran na huku akigusia jinsi serikali ilivyosimama imara kukabiliana na njama za kuzuia au kuakhirisha kufutwa vikwazo hivyo vya kidhulma amesema, hali itabadilika baada ya kuingia madarakani serikali mpya nchini Marekani kama ambavyo hata kama rais wa hivi sasa wa nchi hiyo angelibakia madarakani, vile vile hali ingelibadilika.
Amesema, serikali ya Iran imetumia nguvu zake kuhakikisha kuwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA hayasambaratiki akisisitiza kwamba lengo kuu la rais wa Marekani, Donald Trump lilikuwa ni kuyasambaratisha makubaliano hayo ya kimataifa, lakini ameshindwa.
Amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka kuwa na uhusiano mzuri na nchi zote duniani hasa Russia na China kama ambavyo inapenda kuwa na uhusiano mzuri na Umoja wa Ulaya pamoja na majirani zake wote.
Rais Rouhani amezungumzia pia kuuliwa kigaidi na kidhulma, shahid Mohsen Fakhrizadeh, mwanasayansi bingwa wa nyuklia na masuala ya kijeshi wa Iran na kusema kuwa, mauaji hayo ya kigaidi yamefanywa na watu ambao walitaka kulitumbukiza vitani eneo hili katika siku hizi za mwisho za kuanguka utawala muovu wa Donald Trump huko Marekani. Aidha amesema, shabaha kuu ya utawala wa Kizayuni katika kumuua kigaidi shahid Fakhrizadeh ni kuzusha machafuko katika eneo hili.
Amesema, utulivu na amani ya eneo hili ni muhimu sana kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, lakini pia ni Tehran itatoa majibu yanayostahiki na kwa wakati unaofaa kwa wahusika wote wa jinai hiyo.