Spika Qalibaf: Kukombolewa Quds ni kadhia muhimu mno kwa Iran
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametahadharisha kuhusiana na njama za Marekani na utawala haramu wa Israel za kuyagawa mataifa ya Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi.
Dakta Muhammad Baqir Qalibaf amesema hayo katika mkutano uliofanyya jana kwa njia ya mawasiliano ya Intaneti wa Wakuu wa Kamisheni za Usalama wa Taifa na Siasa za Kigeni za Mabunge ya Nchi Zinazoiunga Mkono Palestina na kubainisha kwamba, kinachofuatiliwa na Marekani na Wazayuni ni kuwafukuza Wapalestina kutoka katika ardhi za mababu zao na kuubomoa msikiti wa al-Aqswa.
Amesema kuwa, kukombolewa Quds Tukufu ni kadhia muhimu mno kwa Jamhuri ya Kiislamu na kwamba, Waislamu wanapaswa kukiunga mkono kibla chao cha kwanza yaani Masjidul-Aqswa hasa kwa kuzingatia kuwa, ni moja ya vitambulisho vya pamoja vya kidini vya Waislamu.
Spika wa Bunge la Iran ameeleza pia, adui amekuwa akifanya njama kupitia vijkwazo, hatua za upande mmoja, vitisho na ubabe kwa ajili ya kutoa pigo dhidi ya umoja wa Umma wa Kiislamu.
Kadhalika amesema kuwa, jinai za kila uchao za utawala wa kigaidi wa Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina hususan wa Ukanda wa Gaza katu hazitafutika katika kumbukumbu za historia.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha pia kwamba, inasikitisha kuona kuwa, jinai zote hizi zinafanyika katika anga ya kimya na misimamo legevu ya baadhi ya watawala wa ulimwengu wa Kiislamu, Umoja wa Mataifa na asasi za kimataifa zinazodai kuwa ni watetezi wa haki za binadamu.