Iran: Trump ameenda, Ghuba ya Uajemi imebakia; alishindwa kutuzuia kuuza mafuta yetu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran iko tayari wakati wote kwa ajili ya mazungumzo na nchi nyingine za Ghuba ya Uajemi kwa ajili ya kulinda usalama na kudumisha amani na ushirikiano katika eneo hili.
Dk Mohammad Javad Zarif amemwambia mwandishi wa habari wa IRIB kwamba, Donald Trump ameenda, lakini eneo la Ghuba ya Uajemi lipo na litabakia na kwamba suala la Iran kupigania mazungumzo ya kuleta umoja, usalama na ushirikiano wa nchi za eneo hili, si jambo geni hata kidogo.
Vile vile amesema, baadhi ya nchi za eneo hili zimepoteza fursa ya miaka minne ya ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi kutokana na siasa za kichochezi wa Donald Trump, lakini sasa Trump ameenda na sisi na nchi hizo tumebakia katika eneo letu hili.
Huku hayo yakiripotiwa, Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, licha ya Donald Trump kufanya njama kubwa za kutaka kuizuia Tehran isiuze nje mafuta yake lakini alishindwa. Trump alijigamba kuwa ataufikisha kwenye sifuri uuzaji wa mafuta ya Iran, lakini kamwe hakuweza.
Bijan Zangeneh, Waziri wa Mafuta wa Iran amesema hayo leo Ijumaa katika sherehe za ufunguzi wa Maonyesha ya 25 ya Mafuta na Gesi humu nchini na kuongeza kuwa, si tu Trump ameshindwa kufikisha kwenye sifuri uuzaji wa mafuta ya Iran, bali Jamhuri ya Kiislamu imeweza kuuza kiwango cha juu zaidi cha mafuta na bidhaa za mafuta katika kipindi cha miaka minne iliiyopita kuliko wakati mwingine wowote.
Aidha amesema, asilimia 70 ya vifaa vya sekta ya mafuta vinatengenezwa ndani ya Iran na licha ya kuzuka janga la corona, lakini Iran imeweza kuchunga protokali za afya na kuendelea kiufanisi na shughuli zake katika sekta ya mafuta na gesi bila kukwamishwa na njama za adui.