Iran yaitaka serikali mpya ya Marekani isisahau kufeli vibaya siasa za Trump
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i66204-iran_yaitaka_serikali_mpya_ya_marekani_isisahau_kufeli_vibaya_siasa_za_trump
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemtaka waziri mpya wa mambo ya nje wa Marekani asiwe mwepesi wa kusahau kufeli vibaya siasa za Donald Trump mbele ya Iran na kusema kuwa, Tehran inaendelea kuheshimu mapatano ya nyuklia ya JCPOA licha ya Marekani kujitoa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 28, 2021 07:50 UTC
  • Iran yaitaka serikali mpya ya Marekani isisahau kufeli vibaya siasa za Trump

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemtaka waziri mpya wa mambo ya nje wa Marekani asiwe mwepesi wa kusahau kufeli vibaya siasa za Donald Trump mbele ya Iran na kusema kuwa, Tehran inaendelea kuheshimu mapatano ya nyuklia ya JCPOA licha ya Marekani kujitoa.

Dk Mohamed Javad Zarif amesema hayo leo Alkhamisi katika mtandao wa kijamii wa Twitter na huku akiashiria uhakika wa kushindwa vibaya mashinikizo ya kiwango cha juu ya Trump dhidi ya Iran amesema, Marekani ndiyo iliyojitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA licha ya kwamba ilikuwa mstari wa mbele kuyafanikisha.

Si hayo tu, lakini pia ni Marekani ndiyo iliyopiga marufuku kuwafikia wananchi wa Iran hata chakula na madawa ya matibabu na kutoa adhabu kwa kila aliyeheshimu azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopasisha makubaliano hayo ya kimataifa.

Antony Blinken, waziri mpya wa mambo ya nje wa Marekani

 

Aidha amemwambia waziri mpya wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken, kwamba, licha ya Washington kufanya ugaidi wote huo dhidi ya taifa la Iran, lakini Tehran muda wote imeheshimu mapatano ya JCPOA na hatua pekee ilizochukua ni zile zilizotabiriwa tangu zamani ndani ya mapatano hayo ambazo upande wowote unaweza kuzichukua iwapo upande wa pili haukuheshimu vipengee vya JCPOA.

Vile vile Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameuliza swali akisema: "Sasa kwa kuzingatia hali hiyo, ni nani hapa anayepaswa kuchukua hatua kwanza?"

Amemwambia waziri mpya wa mambo ya nje wa Marekani kwamba: "Nakushauri usiwe mwepesi wa kusahau kufeli vibaya mashinikizo ya kiwango cha juu ya Trump mbele ya Iran."

Mapema leo asubuhi, Antony Blinken, waziri mpya wa mambo ya nje wa Marekani ametumia mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari tangu ateuliwe kushika wadhifa huo, kuituhumu Iran kuvunja mapatano ya JCPOA.