Abdollahian: Iran ina stratejia maalumu ya kuwaunga mkono Wapalestina
Mshauri maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa amesema Iran ina stratejia maalumu, thabiti na kabambe ya kuwaunga mkono na kuwasaidia wananchi wa Palestina.
Hossein Amir-Abdollahian ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Mkutano wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina, alisema hayo jana katika hotuba yake mbele ya Kongamano la Pili la Kimataifa la Quds Tukufu lililofanyika kwa njia ya intaneti.
Ameeleza bayana kuwa, "kuwahami Waislamu madhulumu wa Palestina, tuna stratejia yenye hekima na thabiti. Badala ya kuwaruhusu Wazayuni kuwepo katika mipaka ya Iran, waitifaki wa Iran wameyazingira maeneo yanayokaliwa kwa mabavu (Israel), na utawala wa Kizayuni umejenga uzio ukihofia muqawama.
Ameashiria hatua ya baadhi ya madola ya Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel na kubainisha kuwa, Siku ya Kimataifa ya Quds inakuja katika hali ambayo, watawala wa nchi chache za Kiislamu kama Imarati na Bahrain, wamesaini makubaliano ya kuanzisha uhusiano na Israel chini ya mashinikizo ya Marekani, wakati ambapo fikra za walio wengi katika eneo wanapinga kitendo hicho.
Kongamano hilo ambalo lilianza jana Jumanne na linamalizika leo limehudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi zaidi ya 30. Miongoni mwa wasomi na wanaharakati wanaozungumza katika kongamano hilo ni kutoka Iran, Palestina, Malaysia, India, Afghanistan, Pakistan, Ufaransa, Argentina, Iraq, Uturuki, Chile, Imarati, Lebanon, Syria, Uingereza, Canada, na Tunisia.
Ikumbukwe kuwa, Imam Khomeini MA, Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitangaza kuwa Ijumaa ya mwisho ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds. Mwaka huu, Siku ya Kimataifa ya Quds itadhimishwa Ijumaa ijayo ya Mei 7.