May 10, 2021 09:30 UTC

Jumamosi usiku, tovuti ya habari ya Yahoo News iliandika makala na ndani yake ilitoa taarifa mpya kuhusu operesheni ya jinai ya kinyama iliyofanywa na jeshi la kigaidi la Marekani ya kumuua shahidi aliyekuwa kamanda wa kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, Luteni Jenerali Qassem Suleimani.

Miongoni mwa yaliyofichuliwa kwenye ripoti hiyo, ni kushiriki kikosi cha Delta Force katika operesheni hiyo ya kigaidi ya kumuua kidhulma Luteni Jenerali Qassem Soleimani na wenzake 9 akiwemo Abu Mahdi al Muhandis, Naibu wa Mkuu wa Harakati ya Kujitolea ya Wananchi wa Iraq, maarufu kwa jina la al Hashd al Shaabi ambayo ina nafasi kubwa katika kupambana na magaidi nchini Iraq.

Jengine lililofichuliwa na ripoti hiyo mpya ya Yahoo News ni wanajeshi magaidi wa Marekani kushirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel katika jinai hiyo na kueleza kwamba, operesheni hiyo itaathiri hali ya kiistratijia ya serikali ya hivi sasa ya Marekani inayoongozwa na Joe Boiden kwenye eneo la Asia Magharibi katika kipindi cha miaka ijayo.

Kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Iraq baada ya kushambuliwa vibaya na Iran

 

Yahoo News imewanukuu maafisa waandamizi 15 wa zamani au wastaafu katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani wakitoa maelezo kuhusu hatua za usalama zilizochukuliwa naWashington kwa ajili ya viongozi wake kwa kuhofia kisasi ambacho Iran ingelipiza na kuongeza kuwa, hatua za usalama kwa baadhi ya viongozi hao zilichukuliwa kimya kimya na kwamba katika bajeti ambayo Trump aliisaini siku za mwishoni mwa mwaka uliopita, aliidhinisha matumizi ya dola milioni 15 kwa ajili ya watu wanaokabailiwa na kitisho kikubwa cha dola la kigeni au maajenti wake.

Christopher Miller, msimamizi wa zamani wa wizara ya ulinzi ya Marekani anasema, hata kama tujaalie kusingelikuwa na lengo la kukabiliana na vitisho, lakini operesheni hiyo ilifanyika kwa tamaa na malengo makubwa zaidi ya kumuua jenerali mmoja wa kijeshi. Kulikuwa na orodha ndefu ya watu ambao jeshi la Marekani lilikuwa limepanga kuwaua.

Donald Trump rais wa zamani wa Marekani aliyefanya jinai kubwa 

 

Katika sehemu nyingine ya ripoti hiyo Yahoo News ambayo imewanukuu maafisa waandamizi wa zamani wa shirika la ujasusi la Marekani CIA, imeelezwa kuwa, katika kipindi cha miaka kadhaa nyuma, shirika hilo na lile la usalama wa taifa la Marekani yalitumia dola milioni mia kadhaa katika miradi ya utafiti ili kufuatilia shughuli za vifaa vya elektroniki na vyombo vya mawasiliano vya Wairani na kudukua na kunasa mazungumzo na mawasiliano aliyokuwa akifanya kamanda shahidi Qassem Soleimani. Hata hivyo maafisa hao hawakufafanua kama gharama hizo kubwa za fedha zilizotumika ziliwezesha kufikiwa lengo lililokusudiwa au la.

Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump ndiye aliyetoa amri ya kuuliwa kigaidi na kijinai Luteni Jenerali Qassem Soleimani. Kamanda Soleimani na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu wa Mkuu wa Hashd al Shaabi ya Iraq pamoja na wenzao 8 waliuawa shahidi kidhulma mapema alfajiri ya siku ya Ijumaa ya tarehe 3 Januari 2020 katika shambulio la kiwoga na la kuvizia la wanajeshi magaidi wa Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad, mji mkuu wa Iraq.

Mike Pompeo, aliyepanga nakushiriki katika jinai za Trump

 

Nukta muhimu katika ripoti hiyo ya Yahoo News ni kule kusema kwake waziwazi kuhusika moja kwa moja Donald Trump, rais wa zamani wa Marekani katika jinai hiyo, na kufichua wazi kwamba Mike Pompeo, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani ambaye aliwahi pia kuwa mkuu wa shirika la kijasusi la nchi hiyo CIA mwaka 2017, naye alishiriki kikamilifu katika jinai hiyo.

Ni vyema tukakumbusha pia hapa kwamba, tarehe 5 Januari 2020, Adil Abdul Mahdi Waziri Mkuu wa wakati huo wa Iraq naye alisema mbele ya kikao cha bunge la nchi hiyo kwamba Luteni Jenerali Qassem Soleimani alikwenda nchini Iraq kwa mwaliko wa serikali na kwa ajili ya kukabidhi ujumbe wa amani wa Iran kwa ajili ya Saudi Arabia.

Kuthibitishwa na viongozi wa Iraq kwamba Luteni Jenerali Qassem Soleimani alikuwa mgeni rasmi wa serikali ya nchi hiyo kwa ajili ya kufikisha ujumbe wa amani wa Iran kwa Saudi Arabia, kulivunja madai yote ya uongo yaliyoenezwa na Trump na serikali yake ya kigaidi kwamba shujaa huyo wa kambi ya muqawama alikwenda Iraq eti kupanga mashambulizi dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani nchini humo.

Hatimaye kama iliyosema ripoti mpya ya Yahoo News, Wamarekani na Wazayuni walikumbwa na hofu kubwa mno baada ya kufanya jinai hiyo. Kwa upande wake Iran nayo ilishambulia vikali kwa makombora kambi kubwa zaidi ya kijeshi ya Marekani nchini Iraq na kubatilisha njama zote zilizokusudiwa kufanywa na wanajeshi magaidi wa Marekani na viongozi wao watenda jinai.

Tags