Iran kuongeza uzalishaji wa mafuta hadi mapipa milioni 6.5 kwa siku
Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema taifa hili limeazimia kuongeza kiwango cha uzalishaji wa mafuta yake.
Bijan Namdar Zanganeh alisema hayo jana Jumatatu pambizoni mwa uzinduzi wa kustawisha kisima cha mafuta cha Azadegan na kuongeza kuwa, "tunaweza kiwepesi kuongeza uzalishaji wa mafuta na kufikia kiwango cha mapipa milioni 6.5 kwa siku."
Waziri wa Mafuta wa Iran ameeleza bayana kuwa, kuongeza kiwango cha uzalishaji wa mafuta ya nchi hii, kutaliletea nguvu taifa hili kiusalama na kiuchumi.

Ameashiria vikwazo vya kiuchumi, kifedha, na kiteknolojia vya maadui dhidi ya Iran na kubainisha kuwa, licha ya vikwazo hivyo, lakini hatua kubwa zimechukuliwa katika kustawisha maeneo yenye utajiri wa mafuta ya nchi hii.
Zangandeh ametoa mfano wa eneo lenye utajiri wa mafuta la Karun Magharibi, ambalo licha ya vikwazo na mashinikizo, lakini limeongeza kiwango cha uzalishaji wa mafuta, kutoka mapipa 70,000 hadi laki nne kwa siku.