Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu kuhusu yanayopaswa na yasiyopaswa katika uchaguzi
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika sehemu ya hotuba yake kwa njia ya televisheni siku ya Ijumaa kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuaga dunia Imam Khomeini MA aliashiria kadhia ya uchaguzi wa rais nchini Iran na ulazima wa kushiriki kwa wingi wananchi katika uchaguzi huo na pia udharura wa wagombea kuwabainishia wananchi masuala muhimu.
Kiongozi Muadhamu alibainisha nukta muhimu na za kistratijia ambazo rais ajae wa Iran anapaswa kuzingatia kuhusu uadilifu wa kijamii, mapambano dhidi ya ufisadi na kuimarisha uzalishaji ndani ya nchi. Kiongozi Muadhamu aliongeza kuwa: "Ikiwa kuna mvurugiko, uzembe na udhaifu katika utawala, hilo linapaswa kurekebishwa wakati wa uchaguzi kwa kufanya chaguo sahihi na zuri na kumkabidhi madaraka msimamizi mwenye kuwajali wananchi na Uislamu. Hali haiwezi kurekebishwa kwa kutoshiriki katika uchaguzi."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliongeza kuwa, utendaji hauwezi kubainika kwa maeneno matupu na hivyo kuna haja ya kutizama uchapakazi wa huko nyuma wa wagombea na iwapo utendaji unaenda sambamba na ahadi zao au la?
Tarajio kutoka kwa kila mgombea ni kuwa, iwapo atapata ushindi atafungamana na uadilifu wa kijamii, atapunguza ufa baina ya masikini na tajiri, atapambana na ufisadi bila mapendeleo, ataimarisha uzalishaji ndani ya nchi na pia kukabiliana na uingizaji bidhaa kutoka nje kwa wingi na kinyume cha sheria.
Ukurasa wa Twitter wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kislamu umetuma ujumbe wa indhari kuhusu kuvunjiana heshima katika midahalo ya wagombea wa urais huku akitoa onyo kali kuhusu suala hilo.
Katika radiamali baada ya mdahalo wa kwanza wa wagombea urais wa Iran uliofanyika Jumamosi alasiri, ukurasa wa Instagram wa Kiongozi Muadhamu pia ulinukulu hotuba yake na kuandika: "Kila wakati ambapo katika midahalo ya televisheni wagombea wanatumia mbinu ya kuvunjiana heshima, kutuhumu na kuharibu jina upande wa pili na kuwatisha wananchi kuhusu mshindani, hilo huwa ni kwa hasara ya nchi."
Kabla ya mdahalo wa wagombea urais pia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia katika ukurasa wake wa Twitter aliwasisitizia wagombea urais kuwa wasibadilishe kampeni za uchaguzi kuwa 'medani ya vita vya madaraka na kuvunjiana heshima' kama invyojiri wakati wa uchaguzi nchini Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya.
Hakuna shaka kuhusu nukta hii kuwa, midhahalo ya wagombea urais nchini Iran italeta msisimuko katika uchaguzi na kuwawezesha wananchi ambao badoa hawajaamua kuhusu mgombea wamtakao kuweza kuamua na kuchukua maamuzi.
Mdahalo ambao unafanyika kwa njia sahihi na kwa kuzingatia maadili unaweza kuwasaidia wapiga kura kuweza kubaini nukta dhaifu na zenye nguvu za mipango ya wagombea katika kipindi hiki kabla ya upigaji kura.
Kwa vyovyote vile baada ya midahalo wasikilizaji na wataalamu katika jamii ndio watakaoweza kubainia ni mgombea yupi mwenye mipango sahihi na ambayo inaweza kutekellezeka. Katika kila uchaguzi kwa kawaida huwa na nguzo mbili, nguzo ya kwanza ni ushiriki wananchi kwa wingi na nukta hiyo huupa uchaguzi uhalali na hivyo kuainisha hatima ya kisiasa ya nchi. Nguzo ya pili katika uchaguzi ni wagombea ambao huwa wanalenga kupigiwa kura na wananchi ili wachukua nafasi za usimamizi katika nchi. Hivyo uchaguzi wa Iran sasa umeweza kuvutia fikra za umma ambapo midahalo ina nafasi muhimu katika medani ya uchaguzi.
Katika siku zilizosalia kabla ya uchaguzi wa rais wa Iran utakaofanyika Ijumaa Juni 18, uwezo wa kila mgombea utaweza kubainika katika kampeni na wananchi wataweza kubaini ni mgombea yupi atakayeweza kukidhi matarajio ya wananchi pindi atakapochaguliwa kuwa rais wa nchi.