Shahram: Iran iko mstari wa mbele kustawisha amani, urafiki kimataifa
(last modified 2021-09-05T02:45:02+00:00 )
Sep 05, 2021 02:45 UTC
  • Admeri Shahram Irani
    Admeri Shahram Irani

Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Admeri Shahram Irani anasema Jamhuri ya Kiislamu iko mstari wa mbele katika kampeni ya kuanzisha na kukuza amani na urafiki wa kimataifa.

Akizungumza Jumamosi na waandishi wa habari pambizoni mwa sherehe ya kufunga awamu ya sita ya mashindano ya kimataifa ya majeshi yaliyopewa jina la "Kombe la Bahari" katika bandari ya kaskazini mwa Iran ya Bandar Anzali kwenye ufukwe wa Bahari ya Kaspi, Admeri Irani ameongeza kuwa Jeshi la Wanamaji la Iran linaipa umuhimu maalumu kadhia ya mawasiliano ya mara kwa mara na mazungumzo kati ya nchi mbalimbali.

Alibainisha kuwa Iran haipiganii nafasi za juu katika mashindano ambayo inashiriki, lakini inakusudia kufanyia majaribio uwezo wa vikosi vyake vya kijeshi katika kiwango cha kimataifa.

"Lengo muhimu zaidi la Jeshi letu la Majini katika Kombe la Bahari ni kukuza diplomasia ya ulinzibaharini," alisema.

Kamanda huyo amesisitiza kuwa Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu linaweza kuanzisha mawasiliano na nchi yoyote yenye mipaka ya maji na kuongeza kuwa Iran inataka "kuongeza na kuimarisha urafiki kati ya nchi."

Awamu ya sita ya "Kombe la Bahari" ilianza huko Bandar Anzali, kwenye Bahari ya Kaspi, mnamo Agosti 25, na askari wapatao 400 kutoka Russia, Jamhuri ya Azerbaijan, Kazakhstan na Iran walishiriki katikia mashindano hayo.

Kulingana na Wizara ya Ulinzi ya Russia, Moscow imepeleka meli mbili katika Bandar Anzali kushiriki mashindano hayo ya Kombe la Bahari ya Michezo ya Jeshi ya Kimataifa ya 2021.

Tags