Ayatullah Jannati: Tunakaribisha kwa mikono miwili mazungumzo ya Iran na Saudi Arabia
Ayatullah Ahmad Jannati, Katibu wa Baraza la Kulinda Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, matatizo ya Ulimwengu wa Kiislamu ni ya kutwishwa na ni matakwa ya mabeberu dhidi ya Uislamu.
Ayatullah Ahmad Jannati amebainisha kuwa, kama tawala na mataifa ya Kiislamu yatadiriki na kufahamu ukweli huu basi badala ya kufikiria kutekeleza mipango ya kishetai na ya mabeberu yatafuatilia suala la umoja na mambo yanayowakutanisha pamoja na hivyo kudhamini maslahi ya Umma wa Kiislamu.
Kadhalika, Ayatullah Ahmad Jannati, Katibu wa Baraza la Kulinda Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza juu ya udharura wa kudumishwa umoja na mshikamano baina ya mataifa ya Kiislamu.
Kuhusiana na mazungumzo ya Iran na Saudi Arabia, Katibu wa Baraza la Kulinda Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuuwa, Tehran inakaribisha kwa mikono miwili mazungumzo hayo.
Ayatullah Jannati amesisitiza kuwa, kama matatizo na hitilafu za nchi mbili za Kiislamu yatapatiwa ufumbuzi bila shaka hiyo itakuwa hatua muhimu.
Hivi karibuni Faisal bin Farhan Aal Saud, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia alinukuliwa akisema kuwa, nchi yake ina nia ya kweli katika mazungumzo yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kabla ya hapo pia, Mohammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia alikuwa amesema kwamba, nchi yake inataka kuwa na uhusiano wa kipekee na mzuri na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.