Iran: Irada ya kisiasa inahitajika kuangamiza silaha za nyuklia duniani
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema irada ya kisiasa inahitajika ili kuangamiza silaha za nyuklia duniani.
Majid Takht-e Ravanchi ameongeza kuwa,baada ya kuanza kutekelezwa Mkataba wa NPT wa Kuzuia Usambazwaji Silaha za Nyuklia mwaka 1970, nchi zilizotia saini ziliahidi kuanza kuangamiza silaha zao za nyuklia. Ameongeza kuwa, pamoja na kuwa baadhi ya madola yameahidi kuangamiza silaha za nyuklia lakini yamejizuia kutekeleza mkataba huo wa NPT kwa visingizo vya kisiasa.
Kwa mujibu wa mkataba wa NPT, nchi zinazomiliki silaha za nyuklia zinapaswa kuangamiza silaha hizo na ziache kutengeneza silaha mpya za nyuklia na pia zijiepushe na kuzuiuzia nchi zingine silaha hizo.
Mnamo Oktoba 28, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliwasilisha pendekezo la azimio la 'Kufuatialia Utekelezwaji wa Mapatano Yaliyofikiwa katika Vikao vya Kujadili NPT vya 1995,2000 na 2010." Pendekezo hilo la Iran limekubaliwa na Kamati ya Kwanza ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa uungaji mkono wa aghalabu ya wanachama.
Azimio hilo litajadiliwa na wanachama wa Baraza Kuu baada ya mwezi moja. Azimio lililopendekezwa na Iran linataka nchi ziliztia saini mkataba wa NPT kuharakisha utekelezaji wa ahadi za kuangamiza kabisa zana zao za nyuklia kwa msingi wa uwazi na usimami wa kimataifa.