Waziri: Marekani haijaonyesha azma imara ya kurejea katika mapatano ya nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i76408-waziri_marekani_haijaonyesha_azma_imara_ya_kurejea_katika_mapatano_ya_nyuklia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Marekani haijaonyesha azma imara ya kutekeleza kivitendo matamshi yake kuwa iko tayari kurejea katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA baada ya mtawala wa zamani wa nchi hiyo Donald Trump kujiondoa katika mapatano hayo mwaka 2018.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 01, 2021 04:44 UTC
  • Waziri: Marekani haijaonyesha azma imara ya kurejea katika mapatano ya nyuklia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Marekani haijaonyesha azma imara ya kutekeleza kivitendo matamshi yake kuwa iko tayari kurejea katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA baada ya mtawala wa zamani wa nchi hiyo Donald Trump kujiondoa katika mapatano hayo mwaka 2018.

Katika mahojiano na gazeti la Iran Jumapili, Hossein Amir-Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria jitihada za kidiplomasia za kuhuisha mazungumzo ya nyuklia na hasa duru kadhaa za mazungumzo zilizofanyika Vienna, Austria  kwa lengo la kuondoa vikwazo vilivyo kinyume cha sheria vya Marekani dhidi ya Iran baada ya nchi hiyo kujiondoa katika mapatano ya JCPOA.

Amir-Abdollahian amesema aliposhiriki hivi karibuni katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Iran ilipokea maombi ya kuitaka irejee katika mazungumzo ya Vienna. Amesema alikutana na wawakilishi wa nchi tatu za Ulaya zilizotia saini mapatano ya JCPOA, yaani Ufaransa, Uingereza na Ujerumani pamoja na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kuwafahamisha kuwa njia bora zaidi ni kuafikiana kurejea katika mazungumzo kwa kuanzia nukta ambayo Trump alijiondoa katika JCPOA.

Amesema, iwapo kweli Marekani inataka kurejea katika JCPOA hakuna haja ya mazungumzo marefu ambayo yamekuwa yakiendelea kwani Rais Joe Biden anaweza kutoa amri ya kurejea katika JCPOA na hali irejee kama ilivyokuwa kabla ya Trump kujiondoa katika mapatano hayo. Amesema hata hivyo tatizo ni kuwa, Marekani inadaiwa kuwa na nia ya kurejea katika mapatano hayo lakini haijatekeleza nia hiyo kivitendo.

Wakati huo huo baada ya kauli hiyo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Rais Biden wa Marekani amesema diplomasia ndio 'njia bora zaidi' ya kuamiliana na Iran. Biden ametoa kauli hiyo baada ya kumalizika kikao cha nchi za G20 huko Roma nchini Italia.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa, mpango wake wa nyuklia ni wa malengo ya amani lakini nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zinatumia kadhia hiyo ya nyuklia kuishinikiza Iran.