Magenge 78 ya magendo ya silaha yasambaratishwa nchini Iran
Wizara ya Usalama wa Taifa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa, imefanikiwa kusambaratisha magenge 78 ya magendo ya silaha na vifaa vya kijeshi humu nchini.
Taarifa hiyo ya Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran ilitolewa jana Jumatatu na kuongeza kuwa, askari wa wizara hiyo wamefanikiwa kusambaratisha magenge 78 ya magendo ya silaha katika kipindi cha miezi 6 iliyopita na kugundua maficho ya magenge hayo. Silaha nyingi zimekamatwa katika operesheni hizo.
Wizara hiyo imetoa ufafanuzi zaidi kwa kusema, katika operesheni hiyo, kumekamatwa silaha 2,170 zikiwemo silaha 473 za kivita, silaha 685 za uwindaji, bastola 782, na silaha nyingine za aina tofauti zipatazo 230.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran, watu 201 wametiwa mbaroni katika operesheni hiyo na kukabidhiwa kwa Idara ya Mahakama.
Hayo yameripotiwa katika hali ambayo, mwanzoni mwa mwezi uliopita wa Oktoba, kamanda wa vikosi vya nchi kavu vya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisisitiza kuwa tangu uje utawala wa Kizayuni karibu na mipaka ya nchi, Iran imezidi kuguswa na suala la usalama wa mipaka yake na kwa sababu hiyo harakati za utawala huo haramu zinafuatiliwa kikamilifu.
Brigedia Jenerali Kioumars Heydari, aliyasema hayo sambamba na kuanza kwa luteka iliyopewa jina la "Wakomboaji wa Khaybar" iliyofanyika katika maeneo ya kaskazini magharibi mwa Iran na kuongeza kwamba, "katika eneo hili tuna mvurugaji wa amani asiyetakikana kuwepo, ambaye amekuja kutokea mahali kwingine, naye ni utawala haramu wa Kizayuni; na tangu utawala huu ulipokuja, tumezidi kuguswa na usalama wetu na tunafuatilia harakati zake kikamilifu."