Raisi katika kikao cha ECO: Vikwazo havitaathiri ushirikiano wa kieneo
Rais Ibrahim Raisi wa Iran amezihakikishia nchi jirani kuwa vikwazo vya Marekani havitaathiri ushirikiano na maingiliano ya kieneo.
Raisi ameyasema hayo Jumapili katika mji mkuu wa Turkmenistan, Ashghabat wakati akihutubia Mkutano wa 15 wa Wakuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya ECO. Katika hotuba yake, Rais wa Iran ametoa wito kwa nchi wanachama kushirikiana katika sekta mbali mbali kama vile soko la pamoja la umeme, miradi ya maji na miradi mingine ya nishati.
Amesema Iran iko tayari kuzisaidia nchi za eneo kuunganisha mtandao wa nyaya za optiki za intaneti na pia kustawisha uga wa teknolojia ya akili ya kubuni au artificial intelligence pamoja na masomo kwa njia ya mtandao.
Halikadhalika Raisi amependekeza kuundwe mfumo wa ndani ya eneo wa kifedha ili kuimarisha ushirikiano wa kuchumi.
Aidha amesema, mbali na kuwa nchi wanachama zina idadi ya watu karibu nusu bilioni, zinamiliki thuluthi moja ya vyanzo vya nishati ya dunia, zina nguvu kazi yenye uwezo na ya vijana, halikadhalika zina nukta moja ya kipekee ambayo ni utambulisho wa Kiislamu. Amesisitiza kuwa, Jamuri ya Kiislamu ya Iran inalipa kipaumbele suala la ushirikiano na nchi za Asia hasa nchi jirani katika eneo la Asia Magharibi, Asia ya Kati na Caucasus.
Nchi wanachaam wa ECO ni pamoja na nchi zote za Asia ya Kati ambazo ni Turkmenistan, Kazakhstan, Tajikistan, Kyrgyzstan, na Uzbekistan pamoja na Afghanistan, Jamhuri ya Azerbaijan, Iran, Pakistan, na Uturuki.