Ebrahim Raisi: Tunafuatilia kwa nguvu kuondolewa vikwazo vyote
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i77702-ebrahim_raisi_tunafuatilia_kwa_nguvu_kuondolewa_vikwazo_vyote
Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema usiku wa kuamkia leo Jumatatu kwamba, Tehran inafuatilia kwa nguvu suala la kuondolewa vikwazo vyote vya kidhulma ilivyowekewa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 05, 2021 23:50 UTC
  • Ebrahim Raisi: Tunafuatilia kwa nguvu kuondolewa vikwazo vyote

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema usiku wa kuamkia leo Jumatatu kwamba, Tehran inafuatilia kwa nguvu suala la kuondolewa vikwazo vyote vya kidhulma ilivyowekewa.

Ayatullah Sayyid Ebrahim Raisi amesema hayo alipozungumza moja kwa moja na taifa kubwa la Iran kupitia televisheni kwa njia ya mahojiano na kuongeza kuwa, leo hii dunia imeelewa kuwa Iran inashiriki kwa nguvu na kwa kulinda vilivyo heshima yake katika mazungumzo hayo ya nyuklia.

Amegusia mapendekezo ya Iran iliyoyakabidhi kwa upande wa pili wa mazungumzo ya Vienna kuhusu kuondolewa vikwazo vya kidhalimu pamoja na kadhia nzima ya nyuklia na kusema kuwa, hadi hivi sasa kumeshafanyika zaidi ya vikao na mawasiliano 100 na wakuu wa nchi tofauti na katika mawasiliano na vikao vyote hivyo Iran imetilia mkazo kuimarishwa mawasiliano ya kijamii, kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi na mataifa ya dunia.

Pande zilizobakia katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA

 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, katika ziara yake ya hivi karibuni ya nchini Tajikistan, pande mbili zimeweza kuimarisha zaidi ushirikiano wao kiasi kwamba baada ya ziara yake hiyo ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi baina ya Iran na Tajikistan umeongezeka mara tatu.

Ayatullah Raisi amezungumzia pia kushiriki kwake kwenye kikao cha viongozi wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai na pia kikao cha wakuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya ECO na kusema kuwa, katika vikao hivyo viwili kulipatikana fursa nzuri ya kuweza Tehran kufungua kurasa mpya za kuimarisha ushirikiano wake na majirani zake na nchi za ukanda huu.