Iran: Lengo la mazungumzo ya Vienna ni kuondolewa vikwazo vyote
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i77706-iran_lengo_la_mazungumzo_ya_vienna_ni_kuondolewa_vikwazo_vyote
Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, lengo kuu la mazungumzo ya Vienna baina ya Iran na kundi la 4+1 na kuondolewa vikwazo vyote vya kidhulma ilivyowekewa Tehran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 06, 2021 03:42 UTC
  • Iran: Lengo la mazungumzo ya Vienna ni kuondolewa vikwazo vyote

Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, lengo kuu la mazungumzo ya Vienna baina ya Iran na kundi la 4+1 na kuondolewa vikwazo vyote vya kidhulma ilivyowekewa Tehran.

Gholam Hossein Esmaili amesema hayo na kuongeza kuwa, Iran ina nia ya kweli katika mazungumzo hayo ya Vienna na lengo kuu la mazungumzo hayo ni Tehran kulinda heshima yake na kuhakikisha vikwazo vyote vinaondolewa.

Amesema, tumeingia kwenye mazungumzo hayo tukiwa tumejipanga vizuri na kwamba Iran iko tayari kuendelea na mazungumzo wakati wowote, lakini pande nyingine zimesema zinahitaji kurejea katika nchi zao kwa ajili ya mashauriano kuhusu mapendekezo yaliyotolewa na Tehran.

Mkuu huyo wa ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, kutokana na mapendekezo yake, Tehran imeonesha ina nia njema na ya kweli ya kutatua matatizo yaliyopo kwenye mapatano ya JCPOA.

Ali Bagheri Kani

 

Itakumbukwa kuwa, Ali Bagheri Kani, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya kisiasa naye amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya al Jazeera kwamba, vikwazo vyote vinavyohusiana na mradi wa nyuklia na vikwazo vyote vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Iran chini ya anwani ya mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa, inabidi viondolewe haraka. 

Amesisitiza kuwa, mapendekezo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kundi la 4+1 katika mazungumzo ya Vienna hayawezi kukataliwa na madola makubwa ya dunia, kwa kuwa misingi yake ni vipengee vya mapatano ya JCPOA yaliyotiwa saini mwaka 2015 na madola hayo hayo.