Iran yalaani shambulizi la kigaidi lililoua raia 30 nchini Mali
Msemaji wa wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, leo Jumatatu asubuhi amelaani shambulio la kigiaidi lililoua raia 30 katika mji wa Mopti, nchini Mali.
Shirika la habari la FARS limemnukuu Saeed Khatibzadeh akilaani shambulio hilo na kusema, Iran inatoa mkono wa pole kwa wananchi na serikali ya Mali kutokana na shambulio hilo la kikatili lililofanywa na magaidi wasio na chembe ya utu na ametaka hatua zichukuliwe za kukomeshwa kabisa vitendo hivyo vya kigaidi.
Wakati huo huo shirika la habari la AFP limetangaza kuwa, miripuko miwili imetokea katika kambi ya Kikosi cha Kulinda Amani ya Umoja wa Mataifa MINUSMA katika eneo la Gao la kaskazini mwa Mali.
Miripuko hiyo imezusha hofu na wasiwasi mkubwa kati ya wanajeshi waliokuwepo kwenye kambi hiyo hasa kutokana na kuwa vitendo vya kigaidi vinatokea mara kwa mara kwenye maeneo hayo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo mkoloni kizee wa Ulaya yaani Ufaransa anaendelea na operesheni yake ya kuhamisha wanajeshi wake kutoka baadhi ya maeneo na kuwapeleka kwenye maeneo mengine.
Kwa mujibu wa mpango huo, Ufaransa imekusudia kuondoa wanajeshi wake katika maeneo mengi ya Mali na kuwaweka zaidi katika maeneo ya mpakani yaani kwenye mpaka wa Mali na nchi za Niger na Burkina Faso.
Tangu mwaka 2012 Mali haijawahi kuwa na utulivu baada ya kutokea mapinduzi ya kijeshi yaliyopelekea kudhoofika serikali kuu na kupata nguvu magenge ya kigaidi kaskazini mwa nchi hiyo likiwemo genge la Daesh.
Licha ya wanajeshi wa Umoja wa Mataifa MINUSMA na wa mkoloni Ufaransa kutumwa huko Mali, lakini machafuko na mashambulizi bado yanaendelea.