Jeshi la Majini la Iran kupata meli tatu mpya za kivita
Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema jeshi hilo hivi karibuni litapokea meli tatu mpya za kivita ambazo ziktakuwa katika bahari za kaskazini na kusini mwa nchi.
Akizungumza Jumatano, Kamanda wa Jeshi la Majini la Iran Admeri Shahram Irani amesema jeshi hilo lina mipango maalumu ya kitaifa na kimataifa.
Admeri Irani amesema Jeshi la Majini la Iran lina mkakati wa kuhakikisha kuwa zana zake zote za kivita za maeneo ya kaskazini na kusini mwa nchi ni mpya. Aidha amesema kwa mujibu wa mpango uliopo uundwaji meli mpya za kivita na zana zinginezo utafanyika ndani ya nchi kutegemea wataalamu Wairani.
Amongeza kuwa manoari ya Damavand itatumwa upande wa kaskazini mwa nchi katika Bahari ya Kaspi na meli zingine mbili za kivita zitatumwa upande wa kkusini mwa nchi katika Ghuba ya Uajemi ikiwemo meli ya kukusanya taarifa za siri yenye uwezo wa kusheheni helikopta. Halikadhalika amesema nyambizi mpia pia inatazamiwa kuanza kutumika katika Ghuba ya Uajemi.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa uwezo wake mkubwa wa kijeshi si tishio kwa nchi jirani bali uwezo huo unadhamini usalama wake na wa eneo.