Duru ya saba ya mazungumzo ya JCPOA kuendelea Vienna leo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i77826-duru_ya_saba_ya_mazungumzo_ya_jcpoa_kuendelea_vienna_leo
Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA) unatazamiwa kuendelea leo mjini Vienna, amedokeza Enrique Mora, Naibu Katibu Mkuu wa Idara ya Hatua za Huduma za Nje (EEAS) katika Umoja wa Ulaya.
(last modified 2026-07-03T11:45:53+00:00 )
Dec 09, 2021 04:46 UTC
  • Duru ya saba ya mazungumzo ya JCPOA kuendelea Vienna leo

Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA) unatazamiwa kuendelea leo mjini Vienna, amedokeza Enrique Mora, Naibu Katibu Mkuu wa Idara ya Hatua za Huduma za Nje (EEAS) katika Umoja wa Ulaya.

Enrique Mora ambaye ni mwenyekiti wa Tume ya Pamoja ya JCPOA ameandika katika ukurasa wake wa Twitter siku ya Jumatano kuwa, "Duru ya saba ya mazungumzo ya JCPOA itaendelea Alhamisi mjini Vienna baada ya wajumbe kuwasiliana na nchi zao zilizo wanachama wa JCPOA.

Duru ya saba ya  kikao hicho cha JCPOA ilianza 29 mwezi uliopita wa Novemba katika mji mkuu wa Austria, Vienna.  Mazungumzo hayo ni baina ya Iran na nchi za kundi la 4+1 kuhusu kuondolewea vikwazo, hasa  vya Marekani dhidi ya Iran. Nchi za 4+1 ni China Russia, Ufaransa, Uingereza, Ujerumani pamoja na mwakilishi wa Umoja wa Ulaya.

Ujumbe wa Iran katika mazungumzo hayo unaongozwa na Ali Baqeri, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni anayeshughulikia masuala ya kisiasa. 

Ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unashiriki katika  mazungumzo huko Vienna kwa mujibu wa haki yake ya kisheria katika fremu ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kile inachotaka ni kuondolewa vikwazo vyote kwa njia ambayo itaweza kuthibitishwa kivitendo.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza mara kadhaa kwamba, lengo kuu la Tehran la kushiriki mazungumzo ya Vienna kuhusu mapatano ya nyuklia ya JCPOA  ni kuhakikisha kuwa taifa hili linaondolewa vikwazo vyote haramu.