Abdollahian ayataka madola ya Magharibi yanayoshiriki mazungumzo ya nyuklia kutekeleza ahadi zao
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i77852-abdollahian_ayataka_madola_ya_magharibi_yanayoshiriki_mazungumzo_ya_nyuklia_kutekeleza_ahadi_zao
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyahutubu madola ya Magharibi yanayoshiriki katika mazungumzo ya nyuklia ya Vienna Austria akiyaambia kwamba, umewadia wakati sasa wa kutekeleza kivitendo ahadi zao.
(last modified 2026-07-02T04:13:23+00:00 )
Dec 10, 2021 01:12 UTC
  • Abdollahian ayataka madola ya Magharibi yanayoshiriki mazungumzo ya nyuklia kutekeleza ahadi zao

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyahutubu madola ya Magharibi yanayoshiriki katika mazungumzo ya nyuklia ya Vienna Austria akiyaambia kwamba, umewadia wakati sasa wa kutekeleza kivitendo ahadi zao.

Hussein  Amir-Abdollahian amesema hayo katika ujumbe wake aliouandika katika mtandao wa kijamii wa Instagram ambapo sambamba na kuashiria kwamba, lengo la mazungumzo ya Vienna Austria ni kufikiwa makubaliano mazuri amesema kuwa, Wamagharibi wanapaswa kutambua kwamba, katika kipindi cha miaka minane iliyopita wamezungumza vya kutosha na sasa ni wakati wa kutekeleza kivitendo ahadi zao.

Abdollahian amesisitiza kuwa, shughuli za miradi ya nyuklia ya Iran ni kwa ajili ya malengo ya amani na kuongeza kuwa, kama upande wa pili utaendelea kushiriki katika mazungumzo hayo kwa nia njema na kwa muono na mtazamo mzuri na wa kujenga na siyo wa kubomoa, bila shaka kutapigwa hatua haraka katika mazungumzo hayo.

 

Aidha katika mazungumzo yake kwa njia ya simu hapo jana na Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisisitiza tena kuwa, taifa hili linafuatilia ili kuhakikisha kwamba, kunapatikana makubaliano mazuri kupitia mazungumzo ya nyuklia ya Vienna Austria kati yake na kundi la 4+1.

Kikao kingine cha Kamisheni ya Pamoja ya Makubaliano ya Nyuklia kilifanyika jana katika mji mkuu wa Austria, Vienna ingawa hadi sasa hakuna makubaliano yaliyofikiwa ambapo Iran inasisitiza kwamba, vikwazo vyote ilivyowekewa vinapaswa kuondolewa kwa mkupuo. Aidha Iran tayari iimewasilisha matini ya mapendekezo yake na lililobakia ni upande wa pili kuchukua uamuzi.